KINARA wa utupiaji ndani ya Klabu ya Azam FC, Prince Dube amesema kuwa viwanja vingi vya mkoani ni vibovu jambo ambalo linawapa ugumu kwenye kupata matokeo na kufunga mabao mengi.
Dube ndani ya Azam FC ambao ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa wamefunga jumla ya mabao 18 amehusika kwenye mabao 10, akifunga sita na kutoa pasi nne za mabao.
Anavutana shati na mzawa, Adam Adam ambaye amefunga jumla ya mabao sita na ni mzawa wa kwanza kufunga mabao matatu,’hat trick’ kwa msimu wa 2020/21 anacheza ndani ya Klabu ya JKT Tanzania.
Adam kwa sasa yupo zake nchini Uturuki na timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ inayojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu Afcon dhidi ya Tunisia, Novemba 13.
Dube alianza kwa kasi kutupia na aliweza kutwaa tuzo ya mchezaji bora ndani ya ligi kwa mwezi Septemba na aliweza kupewa pia na tuzo ya mchezaji bora chaguo la mashabiki kutoka Azam FC kwa mwezi huo.
Nyota huyo amesema:”ushindani kwenye ligi ni mkubwa na kila timu inahitaji kupata ushindi. Kumekuwa na ugumu kwenye mechi zetu za mkoani hasa kwenye upande wa sehemu za kuchezea kuwa ngumu jambo ambalo linatufanya tupate matokoe kidogo tofauti na tukiwa Azam Complex.”
Kwa sasa Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza zimesimama kwa muda kwa kuwa timu za taifa zina majukumu ya kufanya ikiwa ni pamoja na kuwania kufuzu Afcon 2021, Cameroon.