WAKATI jina la kiungo Tonombe Mukoko likitajwa kuingia kwenye rada za watani wa jadi Simba, nyota huyo amesepa na tuzo mbili kutokana na kuwapa tabu wapinzani wake hao Novemba 7, Uwanja wa Mkapa.
Kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulikamilika kwa sare ya kufungana 1-1, huku bao la kuongoza la Yanga likifungwa na Michael Sarpong kwa mkwaju wa penalti na lile la Simba likifungwa na beki Joash Onyango kwa kichwa.
Hiyo ni dabi yake ya kwanza kiungo huyo mwenye nguvu za kupiga mashuti ya nje 18 kuicheza tangu ajiunge na timu hiyo kweye msimu huu akitokea AS Vita DR Congo.
Kiungo huyo tuzo yake ya kwanza kuipata ni ile iliyotolewa na wadhamini wenza wa ligi ambao ni KCB baada ya jopo la makocha wakubwa nchini kumpendekeza kuwa mchezaji bora wa dabi hiyo.
Tonombe aliipata tuzo nyingine kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao walimpigia kura nyingi kiungo huyo zikimchagua kuwa nyota wa mchezo huo dhidi ya Simba ambazo zinaendeshwa kupitia mitandao ya kijamii.
Mkongomani huyo alifanikiwa kupata kura asilimia 54 ya kura zote zilizopigwa akiwashinda beki wa kati Bakari Mwamnyeto na kiungo fundi Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Nyota huyo alijikusanyia kitita cha Sh 2Mil kwa dakika 90, alizozicheza katika dabi hiyo iliyokuwa na upinzani mkubwa kutokwa KCB iliyompa 1Mil na Yanga waliompa 1Mil.
Tangu ajiunge na Yanga katika msimu huu, hii inakuwa tuzo yake ya nne kwa Mukoko kutwaa, kabla ameshatwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara mbili dhidi ya Kagera Sugar na Simba, nyingine tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Septemba na hiyo ya KCB.
Habari zinaeleza kuwa kutokana na uwezo wake kuwa bora baada ya kuibukia Yanga, Simba imeanza kumpigia hesabu kumuongeza kwenye dirisha dogo msimu huu.