IMEELEZWA kuwa mabosi wa Simba wamezinasa mkononi siri zote zinazowahusu wapinzani wao, Plateau United ya Nigeria ikiwemo staa wao matata kabla ya kuvaana nao Jumapili hii mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba wamepata siri hizo ikiwa ni siku chache kabla ya kucheza na Plateau kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, huku wakielezwa, Junior Salomon raia wa Benin ndiye mtu wa kumchunga kutokana na madhara aliyokuwa nayo.
Msafara wa kikosi cha Simba, uliondoka jijini Arusha Jumanne kuelekea nchini Nigeria tayari kwa mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo itakayochezwa wikiendi hii kabla ya ile ya marudiano kati ya Desemba 4-6 jijini Dar.
Tayari imeshatia timu nchini Nigeria jana Jumatano na ilianza kufanya mazoezi ili kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
Habari zimeeleza kuwa wakati walipokuwa wakielekea Nigeria, tayari wana taarifa zote muhimu kuhusu wapinzani wao hao ambapo kocha wa kikosi hicho, Sven Vandenbroeck amepanga kwenda kucheza soka la kushambulia kwa ajili ya kumaliza shughuli ugenini.
“Kwa sasa tuna siri zote za wapinzani wetu Plateau United kabla ya kucheza nao, ikiwemo ya mtu hatari ambaye tunatakiwa kumuangalia zaidi.
“Huyo ni Junior Salomon raia wa Benin ambaye ndiye mtu muhimu kikosini hapo, hivyo lazima achungwe kwa dakika zote.
“Lakini pia wachezaji wanatakiwa kwenda kushambulia na kupata ushindi kwenye mechi hii na kumaliza kila kitu kabla ya kurudi Dar kurudiana nao,” ilieleza taarifa hiyo.