MKOA wa Ruvuma kwa mwaka 2020 utakuwa ni mwenyeji katika Semina ya mafunzo ya mchezo wa Karate Tanzania, (GASSHUKU 2020).
Semina hiyo inatarajiwa kufanyika kuanza Desemba 4 mpaka Desemba 12 mwaka huu wa 2020 huku maandalizi yakiendelea kwa sasa.
Semina na mafunzo hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la mchezo wa Karate Tanzania (JKA/WF-TZ) yamekuwa yakifanyika katika mikoa mbalimbali kila mwaka na mwaka jana yalifanyika mkoani Morogoro na mwaka huu mkoa wa Ruvuma utakuwa mwenyeji.
Lengo kuu la semina na mafunzo hayo ni kuutangaza mchezo wa Karate Tanzania pamoja na kuangalia viwango vya makarateka nchini Tanzania.
Lawrence Mapunda kutoka kurugenzi ya Idara ya Mahusiano na Habari kwa Umma ya Shirikisho la mchezo wa Karate Tanzania (JKA/WF-TZ) amesisitiza kukamilika kwa maandalizi ya GASSHUKU hiyo.
Pia makarateka watapata fursa ya kufanya mitihani ya mchezo huo itakayosimamiwa na mkufunzi mkuu wa mchezo wa karate Tanzania, Sensei Jerome Mhagama Pamoja na msaidizi wake Mikidadi Kilindo.