LEO macho na maskio ya mashabiki wa mpira Bongo kwa muda vitaweka nguvu kubwa Arusha ambapo mashindano ya Cecafa kwa timu za taifa chini ya miaka 20 yanafanyika ambapo ni hatua ya nusu fainali.
Michauano hiyo ilianza Novemba 22 na inatarajiwa kumalizika Desemba 2 kwa fainali kuchezwa kwa wale watakaoshinda leo mchezo wa hatua ya nusu fainali.
Tanzania inawakilishwa na timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes ambao mwendo wao unaleta matumaini ya timu hiyo kufanya vizuri ikiwa itaendelea na morali ya kupambana.
Hapa ni namna mambo yalivyokuwa twende sawa:-
Safari yao
Mechi ya ufunguzi ilichezwa Novemba 22 ambapo Ngorongoro Heroes ilifungua kwa kishindo kwa ushindi wa mabao 6-1 Uwanja wa Black Rhino, Karatu, Arusha kwa kuwashushia kichapo hicho timu ya Taifa ya Djibout.
Watupiaji kwa Tanzania ilikuwa ni Tepsi Theonasy,Abdul Hamis aliyefunga mabao matatu wengine ni Kheleffin Hamdoun na Kassim Haruna hawa walifunga bao mojamoja na lile la kufutia machozi kwa Djibouti lilifungwa na Abdourahman Kamil.
Mchezo wa pili Ngorongoro Heroes ilicheza dhidi ya Somalia, Novemba 26 Uwanja wa Black Rhino ilishinda mabao 8-1 wafungaji wakiwa ni Hamis Seleiman,Ben Stakie, Kelvin Joh alitupia matatu, Kassim Haruna, Frank George na Anuar Jabir walitupia bao mojamoja lile la upinzani lilifungwa na Sahal Muhumed.
Wakali wa hat trick
Ngorongoro Heroes ikiwa imecheza michezo miwili ikiwa nyumbani imefunga jumla ya mabao 14 huku katika hayo mabao imetoa jumla ya wachezaji wawili katika kila mchezo waliosepa na mpira baada ya kufunga hat trick.
Ndani ya dakika 180 imefungwa mabao mawili ambapo safu yao ya ushambuliaji imekuwa na wastani wa kuruhusu bao moja kilabaada ya dakika 90 huku ile ya ushambuliaji ikiwa na hatari kila baada ya dakika 12.
Wa kwanza kufunga ‘hat trick’ alikuwa ni Abdul Hamis alifunga kwenye mchezo wa ufunguzi dhidi ya Djibout na wa pili ni nahodha Kelvin John aliyefunga kwenye mchezo dhidi ya Somalia.
Watengeneza mipango
David Kameta maarufu kama ‘Duchu’ alipiga hat trick ya asisit kwenye mchezo dhidi ya Somalia hivyo yeye anazo tatu kibindoni na Kelvin John ambaye ni nahodha ametoa jumla ya pasi mbili za mabao ilikuwa ni kwenye mchezo wa ufunguzi dhidi ya Djibout .
Hesabu za kocha
Jamhuri Kihwelo, ‘Julio’ ameweka wazi kuwa mpango mkubwa wa timu ya Ngorongoro Heroes ni kuweza kutinga fainali na kuweza kutwaa taji la Cecafa kwa kuwa wapo nyumbani na wanaamini inawezekana.
“Ushindani ni mkubwa na kila timu ambayo inaingia uwanjani hesabu zake ni kupata ushindi hivyo nasi tunapambana kuona namna gani tunaweza kupata matokeo chanya ili tuweze kuwa mashujaa.
“Kikubwa na malengo yetu ni kuona kwamba tunaweza kutwaa ubingwa wa Cecafa hiyo ni hesabu namba moja. Mashabiki waendelee kutupa sapoti kwani vijana wanapambana ndani ya uwanja,” alisema.
Fainali
Ikiwa Ngorongoro itashinda mchezo wake dhidi ya Sudan ya Kusini utakaochezwa Novemba 30 ambayo ni leo ina kibarua cha kukutana na mshindi kati ya Uganda ama Kenya kwenye hatua ya fainali inayotarajiwa kuchezwa NoDesemba 2.
Uganda na Kenya nao pia wanacheza mchezo wa hatua ya nusu fainali leo.
Ngorongoro Heroes itaingia uwanjani ikiwa imeshajua itakutana na nani kwa sababu mchezo wao utachezwa saa tisa na nusu huku mpinzani wake atakuwa ameshacheza saa sita kamili mchana, Uwanja wa Black Rhino, Karatu Arusha.