LICHA ya kupata ushindi kwenye mechi zake mbili mfululizo na kusepa na pointi sita zote mbele ya Azam FC, Novemba 25 na mbele ya JKT Tanzania, Novemba 28 kwa ushindi wa bao mojamoja, Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze amesema kuwa tatizo linalomuumiza ni ubutu wa washambuliaji wake.
Ikiwa ipo nafasi ya kwanza baada ya kucheza mechi 13 na kibindoni ina pointi 31 imefunga mabao 15 ndani ya dakika 1,170 ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 78.
Kinara wa utupiaji wa mabao ndani ya kikosi hicho ni mshambuliaji wake namba moja Michael Sarpong mwenye mabao matatu.
Akizungumza na Saleh Jembe, Kaze amesema kuwa kwa sasa kinachoisumbua safu yake ya ushambuliaji ni kushindwa kumalizia nafasi ambazo wanazitengeneza ndani ya uwanja.
“Kwenye mechi zetu ambazo tunacheza huwa tunatengeneza nafasi nyingi ila wachezaji wangu wengi wanashindwa kuzitumia jambo ambalo inapaswa lifanyiwe kazi haraka.
“Kupata pointi tatu ni jambo la msingi ila ni muhimu pia kupata mabao mengi ili kuongeza hali ya kujiamini ndani ya uwanja, hivyo nina amini baada ya muda litakwisha na tutapata ushindi mkubwa,” amesema Kaze.
Ushindi mkubwa kwa Yanga ilikuwa ni wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union, Okotoba 3, Uwanja wa Mkapa.