SAID Ntibanzokiza nyota mpya wa Yanga amesema kuwa atapambana kufanya vizuri ndani ya kikosi hicho ili kufikia mafanikio aliyonayo pamoja na ya timu kiujumla.
Jana Desemba 3 alianza mazoezi ndani ya Yanga baada ya kutua usiku Desemba 2 akitokea Burundi akiwa ni mshambuliaji mpya ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Cedric Kaze.
Nyota huyo ameweka wazi kwamba anatambua hesabu za Yanga ni kutwaa ubingwa jambo ambalo linahitaji ushirikiano kwa kila mmoja.
“Ninashukuru kuona kwamba nipo ndani ya Yanga, timu kubwa na yenye mipango mikubwa imani yangu ni kwamba tutafikia malengo ambayo tumejiwekea kwa kuwa kila kitu kinawezekana.
“Kikubwa ni kuona kwamba tunashirikiana vizuri na katika hilo ninaamini tutafanya vizuri bila mashaka,” amesema.
Nyota huyo amesaini dili la miaka miwili kwa ajili ya kuitumia timu hiyo na ataanza kutumika ndani ya Yanga kuanzia Desemba 15 baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa.