UONGOZI wa Biashara United umesema kuwa ikiwa mabosi wa Azam FC wanahitaji saini ya kipa wao namba moja Daniel Mgore ni suala la kukaa mezani ili kujadili namna ya kumaliza dili hilo.
Mgore amekuwa ni chaguo namba moja kwa Kocha Mkuu, Francis Baraza alikuwa kikosi cha kwanza Novemba 30, Uwanja wa Karume wakati timu hizo zikigawana pointi mojamoja kwa kufungana bao 1-1.
Seleman Mataso, Mwenyekiti wa Biashara United amesema kuwa hakuna tatizo ikiwa mchezaji atapata ofa nzuri ni jambo la kuongea.
“Imekuwa inaelezwa kwamba Azam FC wanahitaji saini ya kipa wetu, hizo ni tetesi na huwezi kuzuia kwa sababu kila mtu anazungumza kile ambacho anakiskia.
“Ila ikiwa wanahitaji saini ya kipa wetu hatuna tatizo tuna amini kwamba tunaweza kuzungumza na kufikia makubaliano kwa sababu hata sisi pia huwa tunachukuwa wachezaji kutoka timu nyingine.
“Kikubwa ni utaratibu ufuatwe ili kuona kwamba namna gani tunaweza kufikia makubaliano kwani hata sisi pia tunamtegemea katika kazi ila ikitokea akapata timu hakuna tatizo,” amesema.