KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema kuwa anajua kazi ya kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Said Ntibazonkiza ‘Saido’, ndiyo maana alipendekeza asajiliwe huku akiwataka mashabiki wa timu huyo kutulia ili waone ubora wake.
Ntibazonkiza, raia wa Burundi, amejiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka miaka miwili akiwa ni mchezaji huru, licha ya kufanya mazoezi na Vital’O ya Burundi.
Kaze amesema kuwa yeye ndiye aliyependekeza usajili wa mchezaji huyo kwa kuwa anajua ubora wake lakini amewataka mashabiki wa timu hiyo watulie ili waone ubora wake baada ya kuanza mazoezi na timu hiyo.
“Ni mchezaji mzuri, najua kwa nini nilipendekeza aje hapa kwa sababu nafahamu ubora na uzoefu wake, ndiyo tunautaka ndani ya timu yetu na tayari ameanza kuonyesha kitu cha tofauti katika mazoezi ambayo tunafanya.
“Jambo la msingi kwa sasa ni kwa mashabiki wetu kutulia na wampe muda ili waweze kuona kile ambacho anacho ndani ya mechi zetu kwa sababu tunataka kuendelea kubakia juu, nguvu yake inahitajika katika mapambano yetu msimu huu,” amesema Kaze.
Wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Mkapa, Saido alikuwa uwanjani akishuhudia namna mambo yalivyokuwa yanakwenda uwanjani.