LICHA ya Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 jana Desemba 13 na kusepa na pointi tatu mazima mbele ya Mbeya City, uongozi umeshusha lawma kwa waamuzi.
Bao la ushindi kwa Simba lilipatikana kipindi cha Kwanza kupitia kwa nahodha John Bocco aliyepachika bao hilo kwa pasi ya Clatous Chama.
Mwamuzi wa kati jana alikuwa ni Martin Sanya alijitahidi kwenda na presha ya mchezo wa jana kutokana na timu zote kuwa na uhitaji wa pointi tatu.
Mbeya City malengo yao makubwa ni kujinasua kwenye mstari wa kushuka daraja na Simba wao jambo lao ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Mtendaji Mkuu wa Simba, (CEO), Barbara Gonzalez amesema kuwa bado maamuzi ya waamuzi ni tatizo ndani ya Ligi Kuu Bara.
Ushindi wa Simba jana unaipandisha kutoka nafasi ya tatu mpaka nafasi ya pili ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 13.
Yanga ni vinara wakiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 15 na nafasi ya tatu ni Azam FC wenye pointi 27 baada ya kucheza mechi 14.
Mbeya City ipo nafasi ya 16 baada ya kucheza mechi 15 na ina pointi 12 kibindoni.