IMEBAINIKA kuwa kiungo mshambuliaji hatari wa Klabu ya Simba, Luis Miquissone amegoma kuondoka ndani ya timu hiyo licha ya matajiri wa Kiarabu kutoka nchini Misri, Klabu ya Pyramids kuonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.
Pyramid inaripotiwa kuwa tayari kuvunja mkataba wa Luis na Simba kwa kuweka mezani dau linalokadiriwa kufikia shilingi Bilioni 1.5 za Kitanzania.
Akizungumzia ofa hiyo mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema Luis alikaa kikao na Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ ili kujadili dili hilo, lakini akamjibu bosi huyo kuwa ana furaha kuendelea kuitumikia Simba na wala hana mpango wa kuondoka ndani ya timu hiyo kwa sasa.
“Suala la Luis kuhitajika na Pyramid ni kweli lipo na tayari walishaleta ofa ambayo ilijadiliwa kwa kirefu na Mwenyekiti wa Bodi ambapo, Luis alipewa taarifa ya uwepo wa dili hilo.
“Lakini Luis mwenyewe alimwambia MO kwamba bado ana furaha kuendelea kuichezea Simba kwa misimu mingi zaidi na kwa sasa hana mpango wa kuondoka Simba,”.