NAHODHA wa Klabu ya KMC, Juma Kaseja amesema kuwa mashabiki wameona namna maamuzi yalivyokuwa hivyo hana cha kuzungumza kuhusu penalti ambayo waliipata Simba jana, Desemba 16 Uwanja wa Mkapa.
Kwenye mchezo wa jana, Kaseja akiwa langoni baada ya mabeki kuokoa hatari dakika ya 73 hakuwa na chaguo baada ya mwamuzi kuweka kati tuta kwa kile ambacho alidai kwamba kuna mchezaji wa KMC aliunawa mpira huo uliokuwa ndani ya 18.
Bao hilo la ushindi lilifungwa na Meddie Kagere dakika ya 77 baada ya Kaseja kushindwa kuokoa penalti hiyo ya Kagere ambaye amefikisha jumla ya mabao matano ndani ya Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Saleh Jembe, Kaseja amesema kuwa kilichotokea ni sehemu ya mchezo na wanawap pongezi wapinzani wao kwa kuwa wameshinda.
“Tunamshukuru Mungu tumemaliza salama mchezo wetu na hakuna majeruhi kuhusu maamuzi hakuna nitakachoweza kusema ila nina amini kwamba kila mmoja ameona na anajua ukweli upo wapi.
“Kupoteza imeshatokea hatuwezi kubadili matokeo hivyo kinachofuata ni maandalizi kwa ajili ya mechi zetu zijazo, kikubwa mashabiki waendelee kutupa sapoti,” amesema.
Simba inafikisha pointi 32 ikiwa nafasi ya pili huku KMC ikibaki na pointi zake 21 ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.