MABOSI wa Klabu ya Brighton wamevutiwa na uwezo wa nyota wa Manchester United, Dan James jambo ambalo limewafanya wamuweke kwenye hesabu za kumpata kwenye usajili wa mwezi Januari.
Kocha Mkuu wa Brighton, Graham Potter anahitaji huduma ya kiungo huyo mwenye miaka 23 ili kuboresha kikosi chake ndani ya Ligi Kuu England ambayo imekuwa na ushindani mkubwa kwa msimu huu wa 2020/21.
Ripoti zinaeleza kwamba kiungo huyo ambaye alijiunga na Klabu ya Manchester United msimu wa 2019 kwa dau la pauni milioni 17 hajawa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Ole Gunnar Solkjaer na hajaonekana kwa muda wa miezi miwili kwenye kikosi jambo linalowapa nafasi Brighton kuipata saini yake.
Potter anaamini kuwa kutopata namba ndani ya kikosi hicho ni fursa kwake kumpata kiurahisi mchezaji huyo mwenye uwezo ndani ya uwanja kwa kuwa kikosi chake kinapambana kusaka ushindi.
Kwa msimu wa 2020/21 James amecheza jumla ya mechi tatu pekee za Ligi Kuu England huku akionyeshwa kadi moja ya njano, United imecheza jumla ya mechi 12 na ina pointi 23 ikiwa nafasi ya 7.