Home Uncategorized UMAKINI WA WACHEZAJI KWENYE DIRISHA LA USAJILI UNAHITAJIKA

UMAKINI WA WACHEZAJI KWENYE DIRISHA LA USAJILI UNAHITAJIKA

 


DIRISHA dogo la usajili lipo wazi tangu Desemba 16 ambapo litaenda hadi Januari 15, 2021 kwa timu kuweza kuboresha vikosi vyao kulingana na mapungufu ambayo wameyaona.

Hiki ni kipindi ambacho timu zinaruhusiwa kuboresha vikosi vyao katika kuhakikisha zinakuwa imara katika kumalizia msimu huu wa 2020/21.

Ni timu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara ambazo ndizo zinahusika na usajili huu.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), timu ambazo zinaruhusiwa kufanya usajili kipindi hiki ni zile ambazo hazijakamilisha idadi ya wachezaji wanaotakiwa.

Ikiwa bado ni mapema tangu dirisha kufunguliwa, niziase klabu kuwa makini katika kuangalia wapi kuna mapungufu na kuyafanyia kazi.

Mabenchi ya ufundi ndiyo yana jukumu kubwa la kuwasilisha majina ya wachezaji inaowahitaji, kisha uongozi kufanyia kazi katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Itakuwa si vema benchi la ufundi la timu husika likawasilisha mapendekezo ya usajili, kisha viongozi wakafanya wanavyojisikia.

Ikitokea hivyo na timu ikafanya vibaya, lawama zikienda kwa kocha itakuwa ni uonevu, hapa viongozi ndiyo watakuwa na jukumu la moja kwa moja kuingia lawamani.

Kama usajili ukifanyika kwa kufuata mapendekezo ya kocha, naamini timu husika itakuwa imara na kama ikishindwa kufikia malengo, ndipo kocha aingie lawamani.

Nazungumza hivyo kwa sababu huko nyuma tumekuwa tukisikia kelele nyingi kwamba viongozi wanaingilia kazi za makocha kwa kusajili wachezaji inaowataka.

Baada ya kuwasajili, inalazimisha wapewe nafasi ya kucheza wakati wanashindwa kuingia kwenye mifumo ya kocha, hapo lazima mambo yaende ndivyo sivyo.

 

Ifikie wakati makocha waheshimiwe, kile wanachokiwasilisha kwa uongozi kifanyiwe kazi kwa manufaa ya timu.

Hasa kipindi hiki cha usajili ni lazima ufanyike usajili ambao ni mapendekezo ya makocha. Ukifanyika usajili kwa mapendekezo ya viongozi ni ngumu kufikia malengo.

 

Kila mmoja kwa nafasi yake aifanye kazi yake inavyotakiwa, makocha waachiwe jukumu la kufundisha timu inapopendekeza wachezaji wa kusajiliwa, uongozi utimize kile ambacho kocha anahitaji.

SOMA NA HII  EXCLUSIVE: MORRISON ANASEPA YANGA,SVEN ATAKA MABAO YA MITA 20, NDANI YA GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI

 

Zile kesi za viongozi kuingilia kazi za makocha hatutarajii kuzisikia kuanzia sasa, kama kuna viongozi wana tabia hiyo waachane nayo mara moja.

 

Wachezaji nanyi kipindi hiki mnatakiwa kuwa makini, suala la kukimbilia fedha bila ya kuangalia mustakabali wa maisha yenu kisoka hapo baadaye mtafeli.

 

Simulizi za wachezaji wengi kusajiliwa na timu fulani wakiwa moto, kisha kuishia benchi, zipo nyingi na kila kipindi cha usajili zinajirudia, sijui hamjifunzi.

 

Pengine mnaona uwezo mlionao moja kwa moja unaweza kuwafanya kucheza popote pale, kama kweli unaamini kipaji chako, basi hakikisha wakati unasajiliwa, kwenye kipengele mojawapo sema unahitaji kucheza kikosi cha kwanza.

 

Kama kweli timu imeridhika na uwezo wako, basi wanaweza kukusajili kwa kupitia kipengele hicho, lakini kama wakiachana na wewe, basi tambua hapo kuna tatizo.

 

Wachezaji wengi ambao tumeona wanasajiliwa wakiwa wa moto kisha wanaenda kuishia benchi, ni wale ambao wanasajili kwa matakwa ya viongozi na siyo benchi la ufundi.

 

Huu ndiyo muda wa kila mmoja kuwa makini, wachezaji msikurupuke kuhama, viongozi nanyi fanyeni kile makocha wenu wanakihitaji.

 

Nizitakie kila la heri timu zote katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo. Kikubwa umakini unahitajika.