BODI ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, imesitisha mipango ya kumsajili kiungo mkabaji wa Plateau United ya nchini Nigeria, Isah Ndala. Hiyo ikiwa ni siku chache tangu wakamilishe usajili wa kiungo raia wa Uganda, Taddeo Lwanga.
Lwanga amesaini dili la miaka miwili ndani ya Simba na amepewa mikoba ya nyota Gerson Fraga raia wa Brazil ambaye anaendelea kutibu jeraha lake la goti.
Simba katika usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa Desemba 16, mwaka huu, Ndala alikuwepo kwenye mipango yao.
Nyota huyo aliisumbua safu ya kiungo ya Simba wakati walipocheza dhidi ya Plateau kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda amesema kuwa timu hiyo haitasajili kiungo mwingine mara baada ya kukamilisha usajili wa Lwanga.
Kaduguda amesema kuwa wamepanga kusajili wachezaji wawili pekee ambao ni beki wa kati na mshambuliaji namba tisa pekee.
“Ilikuwepo mipango ya kumsajili Ndala lakini hivi sasa haipo tena kwani tayari tumemsajili Lwanga anayecheza nafasi hiyo,” amesema Kaduguda.
Lwanga ambaye ni kiungo mkabaji alikwama jana kucheza kwenye mchezo wa kimataifa dhidi ya FC Platinum kutokana na vibali vyake kuchelewa kufika.
Simba ilinyooshwa kwa bao 1-0 dhidi ya FC Platinum inatarajiwa kurejea nao Januari 6, Uwanja wa Mkapa.