Home Uncategorized MAHAKAMA YAMPIGA ‘STOP’ MORRISON SIMBA

MAHAKAMA YAMPIGA ‘STOP’ MORRISON SIMBA


 MAHAKAMA ya Usuluhishi ya Masuala ya Soka ya Kimataifa (CAS) kumtumia barua ya kumsimamisha kiungo mshambuliaji wa Simba, Mghana, Bernard Morrison kucheza soka hadi pale kesi yake itakaposikilizwa upya na hukumu kutolewa.

 

Hiyo ni baada ya Yanga kupeleka mashitaka yao CAS ikiomba sakata hilo kusikilizwa upya baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumuamuru Morrison kuwa mchezaji huru na yeye kuamua kuibukia ndani ya Simba.

 

Kamati hiyo iliamuru Mghana huyo kuichezea Simba baada ya kubaini mkataba wake wa awali na Yanga kuonekana una mapungufu, maamuzi hayo yaliwafanya viongozi wa Yanga kukimbilia CAS kwenda kukata rufaa.


Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kutoka ndani ya Simba, CAS imemtumia barua kiungo huyo ikimtaka kutoendelea kuitumikia timu hiyo katika mashindano yoyote ikiwemo Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Mtoa taarifa huyo alisema zaidi ya wiki moja na nusu sasa zimepita tangu kiungo huyo mwenye mbwembwe za kuupanda mpira kupokea barua hiyo ya kumzuia kuichezea Simba hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa na hukumu kutolewa na CAS.

 

Aliongeza kuwa, hiyo ndiyo sababu ya Simba kumuacha kiungo huyo kwenye safari ya Mbeya wakati Simba ilipokwenda kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, pamoja na Zimbabwe walipokwenda kucheza dhidi ya FC Platinum katika Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia akiukosa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC.

 

“Ukweli wa Morrison kuachwa kwenye msafara wetu uliokwenda kucheza dhidi ya Mbeya City mkoani Mbeya pamoja na huu wa Zimbabwe ni baada ya kupokea barua kutoka CAS.

 

“CAS walimtumia shauri la kusikilizwa kesi yake upya baada ya Yanga kumkatia rufaa wakiomba kusikilizwa upya kesi hiyo ambayo imekaa vibaya baada ya mahakama hiyo kumsimamisha kuitumikia Simba hadi pale itakaposikilizwa kesi hiyo na hukumu kutolewa.

 

“Hiyo ndiyo sababu kubwa ya Morrison kutokuwa sehemu ya mechi zetu kwa sasa, hakuna kingine,” alisema mtoa taarifa huyo.Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla, alisema: “Suala la Morrison tumelifikisha CAS baada ya TFF kumuamuru mchezaji huyo kuwa mali ya Simba, sisi tumeenda huko lengo ni kupata haki ambayo ninaamini tutapata,” .

SOMA NA HII  MSOME BENZEMA MFALME WA REAL MADRID

 

Morrison ambaye aliitumikia Yanga kwa takribani miezi sita, msimu huu alijiunga na Simba ambapo usajili wake huo ulileta mvutano mkubwa kiasi cha kufikishana TFF ambapo shirikisho hilo lilitoa majibu ya kwamba mchezaji huyo yupo huru kujiunga na timu yoyote baada ya kubaini mapungufu kwenye mkataba wake na Yanga.