IMEELEZWA kuwa wadhamini wa Klabu ya Yanga, kampuni ya GSM imedhamiria kumshusha Bongo mshambuliaji wa zamani wa Klabu ya Angers ya Ufaransa, Ferebory Dore.
Nyota huyo anatajwa kuwa pacha wa Saido Ntibanzokiza ambaye ameshaingia jumlajumla kikosi cha Kwanza akiwa amecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kufunga bao moja na pasi tatu za mabao.
Jina la nyota huyo linatajwa kuwa mikononi mwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hesri Said.
Habari za ndani ya Yanga zinaeleza kuwa nyota huyo tayari ameshamalizana na Yanga ni suala la muda tu kutambulishwa kwa mashabiki na wanachama wa Yanga.
Dore mzaliwa wa Congo mwenye miaka 31 kwa sasa ni mchezaji huru hivyo amejiunga na Yanga bure.
Msimu wa 2009/13 alikuwa ndani ya Klabu ya Angers na alicheza jumla ya mechi 105 na kutupia mabao 11 na alirejea tena msimu wa 2015-18 na alicheza mechi 18.
Injinia Hersi Said amesema kuwa wapo Kwenye mpango wa kumleta Bongo mshambuliaji matata ila jina lake wataliweka wazi hivi karibuni kabla ya dirisha dogo kufungwa.