UONGOZI wa Namungo FC umesema kuwa utapambana kwa hali na mali kusaka matokeo kwenye mchezo wa marudio wa Kombe la Shirikisho dhidi ya El Hilal Obeid ya Sudani.
Namungo tayari imewasili nchini Sudani leo Januari 4 baada ya kuanza safari jana Januari 3 kuwafuata wapinzani wake.
Inatarajiwa kumenyana na Wasudan hao Januari 6 kwenye mchezo wa pili ambapo ina kazi ya kusaka ushindi ili ijiongezee uhakika wa kusonga mbele.
Mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Namungo ilishinda mabao 2-0 ambapo watupiaji walikuwa ni Sixtus Sabilo na Stephen Sey ambaye ana mabao matatu kwenye Kombe la Shirikisho.
Akizungumza na Saleh Jembe, Kocha Mkuu wa Namungo, Hemed Morroco amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo na watapambana kupata matokeo chanya.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchez wetu wa marudio na kila mchezaji nimempa majukumu yake ya kufanya ndani ya uwanja ni matumaini yangu kwamba kila mmoja atafanya vizuri.
“Mashabiki wetu wazidishe dua kwetu nasi tutapambana kupata matokeo ndani ya uwanja,” amesema.