Home Uncategorized TUISAPOTI TAIFA STARS IFANYE VIZURI CHAN

TUISAPOTI TAIFA STARS IFANYE VIZURI CHAN

KUACHA kuipa sapoti Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa namna yoyote ile kwa Mtanzania ni makosa. Tunasema ni makosa kwa sababu hii ni timu yetu wote, hivyo tunapaswa kuipa sapoti.

 

Kwa namna ambavyo tutazidi kuipa sapoti ikiwa inapambana uwanjani, taratibu wachezaji watazidi kuongeza nguvu ya kupambana na kufanya vizuri ndani ya uwanja.

 

Tunaona kwamba awali baada ya Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije kutangaza kikosi wengi walikuwa wanachambua kwa namna ambavyo walikuwa wanajua.

 

Tuliweka wazi kwamba ni muhimu kwa kila shabiki kuweka kando tofauti zake na kukubali kwamba kazi ya kuchagua kikosi ni ya kocha na si ya mtu mwingine.


Kocha kwa sasa anapaswa azungumziwe kuhusu matokeo ambayo ameyapaa ndani ya uwanja. Ipo wazi kwamba kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya DR Congo ulikamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

 

Kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri kwa Taifa Stars kwa kuwa ilishindwa kuonesha yale makali yake, ila kipindi cha pili mambo yalibadilika na hatimaye waliweza kuweka mzani sawa.

 

Kuelekea maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani maarufu CHAN itakayofanyika nchini Cameroon kuanzia Januari 16 hadi Februari 7, mwaka huu, ni muhimu maandalizi yakawa mazuri zaidi ili timu iweze kupata matokeo chanya kwenye mechi zake ambazo ni muhimu kushinda.

 

Kikubwa ambacho tunaamini ni kwamba kila mchezaji amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania jukumu lake kuwa ni kupambana kusaka matokeo mazuri.

 

Tunaamini kwamba mashabiki wanaipenda timu ya Taifa ya Tanzania hivyo kazi yao siku zote iwe moja tu kuipa sapoti timu hiyo bila kuchoka.Kila mchezaji anapenda kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja hivyo pale ambapo wanashindwa kupata matokeo ndani ya dakika 90 lazima wajifunze kwa ajili ya mechi zijazo.Ushindani kwenye timu za Taifa siku zote huwa unakuwa mkubwa kwa sababu kunakuwa na mchanganyiko wa wachezaji tofauti ambao wana uwezo ndani ya timu zao.

SOMA NA HII  SIMBA BANA, YATIMIZA 4G MBELE YA ALLIANCE YA MINZIRO

 

Rai yetu Spoti Xtra kwa Watanzania zile tofauti zao ambazo walikuwa nazo msimu uliopita wa 2020 waziweke kando na kuanza mambo upya.Ikumbukwe kwamba kwa sasa tunaishi ndani ya 2021 na sio 2020 kama ilivyokuwa zamani, hivyo ni muhimu kila mmoja akabadilisha mtazamo na kufanya mambo ambayo yatakuwa na faida kwa Tanzania.

 

Jambo jema ni kwamba kwa sasa tunashiriki michuano hii ya CHAN kwa mara ya pili baada ya awali kushiriki mwaka 2009.Nafasi ambayo tumeipata kwa sasa ni muhimu pia kwa wachezaji kuibeba vyema Bendera ya Taifa na kuipeperusha kwenye mechi zote ambazo watashuka uwanjani.Inawezekana ikiwa watajitoa kwa hali na mali na kufanya kazi kwa juhudi bila kuhofia kwa kuwa uwezo wanao na nina amini watafanya vizuri.