KIUNGO mshambuliaji mpya wa Klabu ya Simba, Perfect Tatenda Chikwende amefunguka kuwa sababu kubwa iliyomfanya atue ndani ya kikosi cha Klabu ya Simba ni kuvutiwa na uwezo mkubwa wa baadhi ya nyota wa kikosi hicho akiwemo Clatous Chama na Luis Miquissone.
Chikwende alitambulishwa rasmi na Simba baada ya kukamilisha dili lake akitokea kwenye FC Platinum ya kwao nchini Zimbabwe.
Chikwende alipata dili hilo baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kwenye michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika waliyocheza dhidi ya Simba ambayo Simba walishinda kwa jumla ya mabao 4-1 huku bao pekee la Platinum likiwekwa kambani na Mzimbabwe huyo.
Chikwende anakamilisha listi ya wachezaji watatu tu ambao Simba imewasajili katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa rasmi Desemba 16 na kufungwa usiku wa Ijumaa ya Januari 15.
Wengine ni Taddeo Lwanga na Junior Lokosa.Akizungumzia kuhusu kumwaga kwake wino ndani ya Simba, Chikwende alisema: “Nafurahi kujiunga na kikosi cha Simba, kila mtu anajua kuwa hii ni timu kubwa, siyo hapa Tanzania pekee bali hata katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
“Miongoni mwa vitu ambavyo vimenivutia kujiunga na Simba ni uwepo wa wachezaji wenye uwezo mkubwa ndani ya kikosi cha Simba, wakiwemo Clatous Chama, Larry Bwalya, Luis Miquissone na Shomari Kapombe.