MAISHA yanakwenda kasi sana na kila siku kuna mambo mapya ambayo yanatokea. Jambo la msingi ni kukubali kwamba hakuna namna ya kuzuia yanayotokea zaidi ni kuendelea kujituma zaidi.
Ikiwa utapoteza kila kitu kwangu naona ni sawa ila usipoteze imani kwa Mungu pamoja na matumaini kwamba kesho utafanya vizuri zaidi ya jana.
Naona rafiki yangu Dickson Job ameamua kusepa ndani ya utawala wake ambao aliujenga kwa muda ndani ya kikosi cha Mtibwa Sugar.
2019 akiwa ndani ya Mtibwa Sugar aliweza kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na nafasi ya kuwa ndani ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20 na alipewa kitambaa cha kuwa nahodha.
Maisha yake sasa yamegeukia pale mitaa ya Jangwani, Job sasa anakwenda kupambania namba na nahodha Lamine Moro,msaidizi Bakari Mwamnyeto hawa wamejenga ufalme wake ndani ya uwanja.
Vitasa hivi ni kwenye Ligi Kuu Bara ngoma ni bandika baundua, Job karibu sana Jangwani ufalme utafahamika tu.
Kuna mwingine anaitwa Juma Makapu na Abdalah Shaibu,’Ninja’ hii nayo ni pacha ambayo ilijibu ndani ya Uwanja wa Amaan, kwenye Kombe la Mapinduzi.
Sasa Job anaingia kwenye changamoto mpya baada ya kuwa ni mfalme ndani ya Mtibwa Sugar akiwa ni chaguo namba moja ndani ya kikosi hicho.
Kwenye mechi 18 ambazo Mtibwa Sugar wamecheza alianza kikosi cha kwanza mechi 17 na alikosekana kwenye mechi moja pekee mbele ya Mbeya City.
Kazi ni moja ndani ya Yanga, Job kuanza kujenga ufalme mpya ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Cedric Kaze.
Sio kazi nyepesi wala sio kazi ngumu jambo ni moja tu kupambana kusaka nafasi kikosi cha kwanza. Yule ambaye anahofia changamoto mpya ni nadra kuona akifanikiwa ila ni namna anaweza kubadili changamoto kuwa fursa kazi ni kwako Job.
Sio Job tu wapo wengi ambao kwenye dirisha dogo wamepata madili na kuingia kwenye maisha mapya wana kazi ya kusaka ufalme kwa kuwapa mashabiki kile ambacho wanahitaji.
Ugumu huwa mwanzo hasa kutokana na kuona mfumo ni tofauti ila mwisho wa siku kazi ya mchezaji ni kucheza tena kikosi cha kwanza na kutimiza majukumu yake.
Ninaona kwamba mpaka Ligi Daraja la Kwanza kuna kazi imefanyika kwa usajili mzuri kwa kila timu kazi kubwa ni kuona kwamba kila mmoja lazima apambane kupata ufalme wake.
Ukigusa pale Simba kuna kichwa kinaitwa Perfect Chikwende, kazi anayo kuufuta ufalme wa Clatous Chama inahitaji akili kubwa na uwezo wa kufanya zaidi ya ambayo anayafanya kwa sasa.
Tuvuke nje ya Dar tuibukie pale Kagera Sugar pana kichwa kinaitwa Yusup Mlipili. Kazi ni moja kwake kusaka ufalme wake mbele ya Ally Mtoni.
Karibu pale Polisi Tanzania kuna mtaasisi anaitwa Kelvin Yondani, mkongwe naona ameshaanza kujenga ufalme wake ni jambo la kusubiri na kuona.