METACHA Mnata, kipa namba moja ndani ya Klabu ya Yanga amesema kuwa kilicho nyuma ya mafanikio yake ndani ya kikosi hicho ikiwa ni pamoja na kutokufungwa kwenye dakika 990 ni ushirikiano wa wachezaji wenzake pamoja na maombi.
Mechi 17 ambazo ni dakika 1530, Mnata alikaa langoni na mechi 11 hakufungwa ambapo ni jumla ya dakika 990 akiwa ni kinara wa ‘clean sheet’ ndani ya makipa wa Bongo anafuatiwa na Daniel Mgore wa Biashara United mwenye ‘clean sheet’ 10 kati ya mechi 15 alizokaa langoni.
Mnata amekuwa chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Cedric Kaze raia wa Burundi amekuwa akimuweka benchi kipa Faroukh Shikhalo ambaye amecheza mchezo mmoja na kufungwa bao moja ilikuwa mbele ya Tanzania Prisons.
Kipa huyo amesema:”Kikubwa ambacho kinanifanya ninakuwa bora ni ushirikiano ambao ninaupata kutoka kwa wachezaji wenzangu pia huwa ninaomba kwani nina amini katika Mungu,” .
Nyota huyo aliibukia ndani ya Yaga akitokea Klabu ya Mbao FC ambapo huko alikuwa kwa mkopo akitokea Klabu ya Azam FC inayonolewa na George Lwandamina.