FISTON Abdoul Razak nyota mpya wa Klabu ya Yanga amesema kuwa Yanga hawatakuwa na haki ya kumzuia kuondoka ikiwa atafanya vizuri ndani ya kikosi hicho baada ya kusaini dili la miezi sita.
Nyota huyo raia wa Burundi amesaini dili la miezi sita katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15,2021 kwa ajili ya kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Cedric Kaze.
Anaungana na nyota mwingine, Saido Ntibanzokiza ambaye naye pia ni raia wa Burundi ambaye huyu anatajwa kusaini dili la miaka miwili.
Habari zinaeleza kuwa Fiston ambaye ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kucheza pia nafasi ya winga anasubiri dili lake jingine litiki nchini Kuwait.
“Miezi sita kwangu ni sawa itanipa fursa ya mimi kuondoka bila kuzuiwa pale ambapo nitahitaji hivyo nina amini nikifanya vizuri itakuwa njia kwangu ya kuondoka.
“Ila kwa namna ambavyo nimeiona Yanga nina amini nitaongeza mkataba mwingine wa kusalia ndani ya kikosi hicho,” amesema.
Yanga ambao ni mabingwa wa Kombe la Mapinduzi kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wapo nafasi ya kwanza na pointi zao ni 44.