BEKI mpya wa kati wa klabu ya Yanga, Dickson Job amefunguka kuwa ameamua kuchagua jezi namba tano ndani ya klabu hiyo kama sehemu ya kumuenzi mtangulizi wake, Kelvin Yondani.
Job alikamilisha rasmi usajili wake wa kujiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili akitokea kikosi cha Mtibwa Sugar ya Morogoro, aliyoichezea kwa mafanikio makubwa kiasi cha kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Star
Anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Yanga kutokea Mtibwa Sugar msimu huu baada ya beki wa kulia, Kibwana Shomari aliyesajiliwa mwezi Agosti.
Job jana alikuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji wa Yanga walioingia kambini kuanza rasmi maandalizi ya michezo ya mzunguko wa wa pili wa ligi inayotarajiwa kurejea mwezi Februari.
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa kuchagua jezi namba tano, Job alisema: “Kama mchezaji wa nafasi ya ulinzi wa kati nimekuwa nikitumia muda mwingi kujifunza kwa watangulizi wangu hasa Kelvin Yondani mchezaji ambaye binafsi nampenda na nimekuwa nikimfuatilia na kujifunza vitu vingi kutoka kwake.
“Yondani amefanya mambo makubwa akiwa na kikosi cha klabu za Simba na Yanga lakini pia akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars hivyo nami kama mchezaji mwenye malengo ya kufanikiwa na kufika mbali ningependa kufuata nyayo zake na ndiyo maana nimechagua jezi aliyokuwa akiivaa nikiamini naweza kuendeleza heshima aliyoiacha.”