KIKOSI cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes kimeibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Al Hilal kwenye mchezo wa Simba Super Cup.
Ikiwa ni mchezo wa kwanza kwa Gomes ambaye amerithi mikoba ya Sven Vandenbroeck ambaye ametimkia Morocco katika Klabu ya FAR Rabat alishuhudia uwezo wa nyota wake ikiwa ni pamoja na Rarry Bwalya aliyeanza kupachika bao la kwanza dakika ya 39.
Bao hilo lilisawazishwa na Salim Mohamed wa Al Hilal baada ya mabeki wa Simba kufanya uzembe huku Beno Kakolanya akishindwa kuokoa mchomo wa kichwa dakika ya 45.
Kipindi cha pili Perfect Chikwende alipachika bao la pili dakika ya 72 baada ya kipa wa Al Hilal kutema shuti lililopigwa na Bernard Morrison ambaye aliingia kipindi cha pili.
Morrison aliweza kufunga mabao mawili ambapo bao la tatu likiwa ni la pili kwake alifunga dakika ya 86 na lile la pili kwake likiwa la nne kwa Simba alifunga dakika ya 89.
Kocha Gomes amesema kuwa wachezaji wake walipambana kusaka ushindi jambo ambalo limewafanya waweze kuibuka na ushindi huo.
“Wachezaji wamepambana kusaka ushindi na wamefanikiwa hivyo naona kwamba wanastahili pongezi kwa kile ambacho wamekifanya,” .