SARE ya mabao 2-2 kwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars itatufangashia virago jumlajumla kwenye michuano ya Chan, nchini Cameroon.
Mabao kwa Tanzania yalifungwa na Baraka Majogoro dakika ya 23 ambapo alikuwa akiweka usawa lile la Barry Yacouba lililopachikwa dakika ya 5 kwa mkwaju wa penalti.
Dakika 45 zilikamilika kwa timu zote kutoshana nguvu na kuwafanya waende kwenye vyumba vya kubadilishana mawazo kila mmoja akiwa na pointi moja na bao moja.
Kipindi cha pili Stars walipata bao dakika ya 67 kupitia kwa Edward Manyama ila halikuweza kulindwa mpaka dakika ya 90.
Lilidumu kwa muda wa dakika 15 ambapo dakika ya 82 Guinea waliweka mzani sawa kupitia kwa Victor na kuongeza mzigo kwa Stars.
Inakuwa ni mara ya pili Stars inayonolewa na Kocha Mkuu, Etiene Ndayiragije kushiriki Chan na kutolewa kwenye hatua ya makundi.
Inatolewa ikiwa na pointi nne kwa kuwa mchezo wa kwanza ilipoteza mbele ya Zambia kwa kufungwa mabao 2-0 na ikashinda bao 1-0 mbele ya Namibia ambao nao pia wamesepa kwenye michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wa ndani.