Home Ligi Kuu MASTAA HAWA KAZI WANAYO

MASTAA HAWA KAZI WANAYO

UKURASA wa mwisho wa kitabu cha usajili Bongo ulifunikwa Ijumaa iliyopita saa 5:59 ambao ndiyo ulikuwa muda wa mwisho kwa timu zote kusajili.

Ndani ya wakati huo kuna nyota ambao wameondoka na kwenda kuanzisha maisha sehemu nyingine. Huko walipoenda kuna kazi ambayo wanatakiwa kuifanya kwa ajili ya kupata upenyo wa kucheza.

Orodha ya wachezaji hao iko ndefu lakini kwenye makala haya inakutajia baadhi yao ambao wana changamoto kubwa ya kuifanya kwa ajili ya kucheza. Twende sawa;

Dickson Job

Ni ingizo jipya ndani ya Yanga inayonolewa na Cedric Kaze raia wa Burundi. Huyu alikuwa ni tegemeo ndani ya Mtibwa Sugar akiwa amecheza jumla ya mechi 17 kati ya 18 za Ligi Kuu Bara.

Kwenye makazi yake mapya anakutana na muziki wa mabeki wanne ambao ni; Bakari Mwamnyeto ambaye pacha yake imejibu na Mghana, Lamine Moro wengine ni Juma Makapu na Abdalah Shaibu ‘Ninja’.

Kazi yake ya kwanza ni kupambana kuvunja moja ya pacha hizo mbili kisha kugombea kuiingia kikosi cha kwanza huku akipambana na watu ambao wamemzidi umri.

Fiston Abdoul Razak

Straika huyu ndiyo kwanza ameingia ndani ya Yanga na ujio wake unaifanya Yanga kutimiza jumla ya washambuliaji watano ndani ya kikosi hicho chenye maskani yake Jangwani.

Anakutana na Ditram Nchimbi, Yacouba Songne, Wazir Junior na Michael Sarpong ambao wapo wanapambania namba kikosi cha kwanza.

Fiston kazi yake kubwa ni kusawazisha makosa ya wenzake ya kukosa mabao kwa kufunga lakini kumshawishi kocha Cedric Kaze kumpeleka moja kwa moja katika 11 ya watakaokuwa wanaanza. Fiston atapambana na Sarpong mwenye mabao manne ambaye ndiye chaguo la kwanza la Kaze.

Perfect Chikwende

Mwamba huyu raia wa Zimbabwe aliwafanya mashabiki wa Simba wasilale kwa kuwa alitambulishwa usiku mnene majira ya saa 11:59. Akiwa ametoka zake FC Platinum anakutana na Miraji Athuman ‘Sheva’ ambaye amerejea kwenye ubora wake.

Sheva ambaye ni mfungaji bora wa Kombe la Mapinduzi akiwa ametupia mabao manne amewaka sawa na Francis Kahata ambaye naye amerejea kwenye ubora.

kushawishi benchi la ufundi kufanya kazi ya ziada kupata namba kikosi cha kwanza.

SOMA NA HII  VIDEO: MKANDALA AJIVUNIA KUWAFUNGA SIMBA MARA MBILI

Mathias Kigonya

Kipa mfungaji raia wa Uganda alisajiliwa na Azam kwenye siku za mwishomwisho za usajili na kufanya kikosi hicho kiwe na makipa wanne.

Makipa hao ni Benedict Haule, David Kissu, Wilbol Maseke na Kigonya. Watatu hao tayari walikuwa wanacheza hivyo Kigonya anahitajika kufanya kazi ya ziada kwa ajili ya kumshawishi Kocha wake mkuu, George Lwandamina kumfanya awe chaguo lake lwa kwanza.

Raphael Daud

Hakuwa ndani ya uwanja kwa muda mrefu akimisi mzunguko wote wa kwanza baada ya kuachwa na Yanga mwanzoni mwa msimu ambapo kwa sasa ameibukia Ihefu SC ya Mbeya.

Kilichopo mbele yake kwa wakati huu akiwa anasubiri kuvaa jezi ya klabu yake hiyo mpya ni kumuaminisha Kocha Mkuu, Zuber Katwila kwamba bado yupo, lakini kuinusuru Ihefu kutoka mkiani mwa ligi.

Peter Manyika

Ndani ya Polisi Tanzania hakuwa na nafasi kutokana na ushindani wa namba. Amesepa zake na kutua Dodoma Jiji ambapo nako ana kazi ya kumpiku Aron Karambo ambaye ni chaguo namba moja la Mbwana Makata.

Akishindwa kufanya hivyo basi kile ambacho alikikimbia Polisi huenda kikajirudia kwa kuwa na urafiki na benchi.

Stamili Mbonde

Hakuwa na timu baada ya kuachwa na Mtibwa Sugar mwishoni mwa msimu uliopita, sasa anaibuka ndani ya Tanzania Prisons inayotumia Uwanja wa Nelson Mandela.

Anakwenda kusaka nafasi mbele Jeremiah Juma ambaye ni mshambuliaji chaguo namba moja la kocha Salum Mayanga.

Yahya Zayd

Kiungo huyu mshambuliaji kazi yake kubwa ni kusaka nafasi ya kucheza ili mabosi wake waliomchukua kwa mkopo Azam FC wasione kwamba ni mzigo na mabosi wake wa Misri, Pharco washtuke kwamba mwamba huyu anayaweza uwanjani.

Erick Kwizera

Wanamuita Messi wa Burundi ambaye aliuwasha kwelikweli kule Mapinduzi Cup na kuwafanya mabosi wa timu hiyo kumpa mkataba. Sasa baada ya kula maisha ana kazi ya kufanya ya kupambana kucheza kikosini lakini kuifanya timu hiyo iwe tishio Afrika.

Ataanza kutumika katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Namungo wamepangwa kucheza na C.D. Primeiro de Agosto ya Angola na kwenye ligi.