UONGOZI wa Yanga umesema kuwa benchi lao la ufundi lipo imara jambo ambalo wanaamini kwamba litawapa matokeo mazuri kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara pamoja na mashindano mengine.
Tayari kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Cedric Kaze kinaongoza ligi kikiwa nafasi ya kwanza na pointi zake kibindoni ni 44.
Kimecheza jumla ya mechi 18 na hakijapoteza mchezo hata mmoja zaidi ya kushinda mechi 13 na kulazimisha sare tano ndani ya uwanja.
Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema kuwa wamejipanga kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mechi zao zote za ligi kutokana na benchi lao imara.
“Tuna benchi makini la ufundi ambalo lina vijana watupu mpaka wachezaji pia asilimia kubwa ni vijana hivyo imani yetu ni kuona kwamba tunafanya vizuri.
“Kikubwa ambacho kipo kwenye mpango wetu ni kupata matokeo tunahitaji kutwaa Kombe la Ligi Kuu Bara, tunahitaji Kombe la Shirisho hilo lipo wazi ni suala la muda tu,” .
Mikoba ya kocha msaidizi ambayo ilikuwa mikononi mwa Juma Mwambusi kwa sasa ipo chini ya mzawa Nizar Khalifan.