Home Habari za michezo KISA YANGA KUFANANISHWA NA PAMBA JIJI…GAMOND ‘AMTEMEA CHECHE’ UCHEBE…

KISA YANGA KUFANANISHWA NA PAMBA JIJI…GAMOND ‘AMTEMEA CHECHE’ UCHEBE…

Yanga SC

BAADA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars na kupanda kileleni, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema kikosi chake hakitakiwi kufananishwa na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sababu hazifanani viwango.

Matokeo ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar juzi usiku yameifanya Yanga kufikisha pointi 24 na kuongoza ligi hiyo huku Singida Black Stars iliyokaa kileleni kwa muda mrefu kushuka hadi nafasi ya pili ikisalia na pointi zake 22 kibindoni.

Yanga ndio timu pekee mpaka sasa haijapoteza mechi hata moja, ikishinda michezo yake yote nane iliyocheza msimu huu.

Gamondi alisema hayo akionekana kujibu kauli iliyotolewa na Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Patrick Aussems, ambaye kabla ya timu hizo kukutana alisema wamejiandaa kuikabili Yanga kama walivyojiandaa kucheza na Pamba Jiji.

Raia huyo wa Argentina amewataka baadhi ya makocha na mashabiki wa soka nchini kuacha kuifananisha Yanga na timu nyingine kwa sababu ubora wa mabingwa hao watetezi umewaacha mbali sana.

Kocha huyo alisema huu ni wakati wa watu kuiheshimu Yanga na wasiifananishe na timu zao kwa sababu mchezo wa mpira wa miguu unamalizikia ndani ya uwanja baada ya ‘maneno mengi’ ya nje.

“Kuna wakati watu wawe wanaiheshimu Yanga, huwezi kutufanisha sisi na Pamba Jiji, mimi naheshimu timu zote, hata hao Pamba Jiji nawaheshimu, lakini wajue mchezo unamalizika ndani ya uwanja sio kuongeaongea nje,” alisema Gamondi.

Kuhusu mchezo huo, Gamondi alisema ulikuwa mzuri na mgumu na kikosi chake kilitengeneza nafasi tano za kufunga kama wangekuwa makini, lakini akisifia kiwango bora ambacho wamekionyesha baada ya muda mrefu kupita.

“Ilikuwa ni mechi nzuri na ngumu, tulitengeneza nafasi tano za kufunga, leo (juzi), tulikuwa katika kiwango bora sana,” alitamba kocha huyo baada ya ushindi huo.

Naye Aussems alikiri kufungwa kihalali, akifurahia na kujitoa kwa wachezaji wake ambao walionyesha upinzani mkali na hiyo imempa ‘kiburi’ bado wapo katika mbio za ubingwa msimu huu licha ya kupoteza mechi hiyo ya juzi.

“Tumeruhusu bao, lilikuwa zuri tu, katika mchezo huu tulikuwa tumejipanga vizuri, wachezaji walikuwa na muunganiko na ushirikiano, hasa kipindi cha pili.

Tulifanya inavyowezekana, lakini haikuwa rahisi kama tulivyokuwa tukifikiria, tulishambulia kutaka kupata mabao lakini tulishindwa na huo ndiyo mpira,” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Aliongeza kupoteza mechi hiyo bado haijawafanya kukata tamaa ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

“Hatujajitoa katika njia ya kwenda kuusaka ubingwa, bado tuna matumaini makubwa ya kuwa mabingwa wa nchi hii, na kiwango cha mchezo wa leo (juzi), kimetufanya tuone kumbe inawezekana,” Aussems aliongeza.

Bao la kiungo mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua, lililofungwa dakika ya 67, liliifanya Yanga kuendelea kupata ushindi wa asilimia 100 msimu huu.

Yanga itashuka dimbani tena kesho kuwakaribisha Azam FC wakati leo Mashujaa itawaalika Simba kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani, Kigoma.

SOMA NA HII  BREAKING: YANGA YAMALIZANA NA BEKI KISIKI WA KAZI