Home Ligi Kuu ISHU YA WAAMUZI TUNALIA NA YAI LENYEWE BILA YA KUANGALIA KIINI…

ISHU YA WAAMUZI TUNALIA NA YAI LENYEWE BILA YA KUANGALIA KIINI…

NA SALEH ALLY

MOJA ya kilio kikuu cha wapenda soka nchini ni waamuzi, vilio vinapishana lakini ndiyo vinabaki kuwa ni vilio vya aina tofauti.

Wanaolia wako kwa upendo na wako kwa malalamiko, mwisho wote wanakuwa na vilio vya waamuzi wa soka hapa nchini.

Binafsi bila ya kupindisha nianze kwa kusema naheshimu sana mchango wa waamuzi katika mchezo wa soka nchini. Wanajitahidi kadiri ya uwezo wao na kuna mambo wamekuwa wakifanya, hakika yanapaswa kupongezwa.

Kwa maana ya wale waamuzi wamekuwa wakiifanya kazi yao kwa weledi, wamekuwa wakijitoa na kufanya mchezo wa soka uendelee.

Tukubaliane, hakuna mwamuzi, hakuna nafasi ya mchezo wa soka kuchezwa. Waamuzi wameifanya Ligi Kuu Bara kuwa maarufu barani Afrika. Lakini swali, likawa vipi kunapotokea kuna suala la uteuzi wa waamuzi kuchezesha michuano fulani ya kimataifa, wa hapa kwetu inakuwa shida?

Mfano, kuna michuano chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), aghalabu kuwa na mwamuzi hata mmoja wa Tanzania, lakini hata kwa wale wanaoteuliwa katika michuano chini ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), huku ndiyo kabisa, maana inajumuishwa dunia nzima?

Shida yetu nini hasa, vipi inakuwa hivi? Kwamba kila mara wanachagua waamuzi wa nchi nyingine na sisi tunakuwa hatuna nafasi hata kidogo!

Kibaya zaidi ni kwamba wakati watu wanachaguliwa, sisi Tanzania hatupo lakini kuna nchi ambazo zimekuwa zikitoa waamuzi mara kwa mara hadi inanishangaza. Burundi na Somalia lakini hata Rwanda.

Unajiuliza vipi Somalia, maana waamuzi kutokea Mogadishu, ligi yao ikoje na ina ubora gani na wao wawe na waamuzi bora kuliko sisi?

Achana na hao, jiulize kuhusiana na Burundi, hawawezi kuwa na ligi bora kama yetu. Vipi watoe waamuzi bora kuliko tulionao, au kuna tatizo? Hali kadhalika Rwanda wanajitahi kuwa na ligi nzuri lakini bado haijafikia hii ya Tanzania Bara, sasa nao wanatuzidi?

Tunazidiwa karibu na kila upande ambao unaona kabisa ligi zao si bora hata kidogo. Hii iimekuwa ikinipa maswali kama ambavyo Watanzania wengi wapenda soka wamekuwa wakijiuliza.

SOMA NA HII  VPL: JKT TANZANIA 0-2 YANGA

Bahati mbaya sana watu wengi wamekuwa wakiamua kuangukia katika lawama zaidi lakini mimi naona kuna mambo mawili makubwa hapa ambayo yanatokea na huenda yakawa ni sababu kubwa ya hili.

Kwanza kabisa, kwao Caf ikiwezekana na Fifa ambapo wanafanya kazi kama ‘chain’ kwa maana ya mnyororo. Zile kamati za waamuzi za mashirikisho haya mawili, bila shaka zinashirikiana kwa ukaribu sana. Hivyo waamuzi wengi wanaichaguliwa na Caf kuna wepesi wa kufanya kazi na Fifa.

Tumeona wataalamu wao hutumwa na kuja kukagua ubora wa waamuzi wetu. Hawa wanaokagua huenda pia huwa na hisia au mazoea, kwamba waamuzi wa Tanzania wako chini kwa kiwango muda wote.

Hivyo, linapofikia suala la kuchagua, labda hawatilii maanani Tanzania, labda wanaona hawataweza na kadhalika. Kuna haja ya TFF na kamati ya waamuzi kuhakikisha kuna utaratibu ubora unaoweza kuwafanya wahusika waone kila kilicho sahihi kinachotokana na waamuzi tulionao.

Pili, ni suala la waamuzi wetu kufundishwa na watu ambao hata kama waliwahi kuwa waamuzi bora wakati huo, huenda kuna vitu wanakosa katika kipindi hiki.

Anza kujiuliza, tuna waamuzi wangapi bora ambao waliwahi kuchezesha angalau Afcon au Chan? Tunao wangapi ambao wamewahi kuchezesha Kombe la Dunia hata la wanawake, vijana au lile kubwa?

Kama hatuna tatizo, kama wapo ubora wao ulikuwa wa kiwango sahihi, walichezesha mara ngapi na je, kwa sasa wana mafunzo ya kuongeza ujuzi zaidi. Maana tunaweza kuwa tunalia na mayai yenyewe, kumbe tatizo likawa mtaga mayai.