STRAIKA wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu amesema kuwa licha ya kuwa na heshima kubwa juu ya mchango wa klabu ya Yanga katika maisha yake ya soka, lakini anapocheza dhidi yao hana budi kuwa kikazi zaidi.
Katika mchezo wa sare ya mabao 3-3 ya mchezo wa Yanga dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam Jumatano iliyopita Mhilu alifunga bao la tatu la Kagera Sugar dakika ya 45 ya mchezo na kuonyesha ishara ya kuomba radhi.
Bao hilo limemfanya Mhilu kufikisha mabao sita msimu huu hivyo kuachwa kwa mabao matatu tu dhidi ya kinara wa ufungaji Meddie Kagere mwenye mabao tisa.
Akizungumzia bao alilowafunga Yanga, Mhilu amesema: “Najisikia furaha kuwa sehemu ya wachezaji walioisaidia timu yangu kupata matokeo ya sare ya ugenini mbele ya Yanga kupitia bao nililofunga.
“Nilionyesha ishara ya kuwaomba radhi Wanayanga baada ya kufunga kwa sababu ni ndani ya klabu hiyo niliweza kulelewa hivyo nathamini mchango wao, lakini wanapaswa kujua kuwa ninapokutana nao ninakuwa kazini na lazima niisaidie timu yangu,”