KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule amesema kuwa bado wana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara licha ya kushindwa kupata matokeo kwenye mechi zao zilizopita.
Mchezo wake uliopita Uwanja wa Azam Complex ilikubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Azam FC na kuifanya iyeyushe jumla pointi sita kwa Azam FC.
Walipokutana mzunguko wa kwanza, Uwanja wa Sokoine, Mbeya City ilikubali kichapo cha bao 1-0 na walipowafuata Chamazi ngoma ilikamilikwa kwa mabao 2-1.
Lule amesema kuwa wachezaji wake wapo imara na wanatambua kwamba wana kazi ya kufanya kutokana na kuwa kwenye nafasi ambayo haina afya kwao ndani ya ligi.
“Wachezaji wanatambua kwamba tuna kazi kubwa ya kufanya ndani ya uwanja hivyo kukosa kwetu matokeo ndani ya uwanja ni darasa.
“Tunaamini kwamba mechi zetu zijazo tutafanya vizuri,mashabiki watupe sapoti tutarejea kwenye ubora wetu,”.
Mbeya City ipo nafasi ya 17 ikiwa imekusanya jumla ya pointi 15 baada ya kucheza mechi 20 na Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 20.