Home Ligi Kuu WAAMUZI UMAKINI UNAHITAJIKA KWA KUWA ILE LADHA YA MPIRA INAPOTEZWA

WAAMUZI UMAKINI UNAHITAJIKA KWA KUWA ILE LADHA YA MPIRA INAPOTEZWA


 HONGERENI Namungo FC kwa kupata ushindi mbele ya 1 de Agosto mkiwa ugenini kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex mkiwa ugenini.

Pongezi kwa kocha Hemed Morocco ila ninaamini kwamba atakuwa na kazi ya kuboresha umakini wa safu yake ya ulinzi ambayo imekuwa ikifanya makosa ya kujirudia ndani ya uwanja.

Bado kete moja mkononi kwenu mkamilishe hesabu za kutinga hatua ya makundi ila bado inapaswa kupambana ili kupata ushindi kwa kuwa dakika 90 kwenye ulimwengu wa mpira ni nyingi.


Kete hiyo ya pili ni leo mkiwa mna kazi ya kusaka sare ama ushindi ili muweze kuhakikisha safari ya kutinga kwenye hatua ya makundi ambapo tayari mshalitambua aina ya kundi ambalo mtakuw mpo hivyo kazi ni kwenu na nafasi ipo mikononi mwenu.

 Nina amini kwamba kila mchezaji anajua kwamba kuna jambo linahitajika kufanyika ili kuwa bora hivyo muhimu kukazana.

Kwa upande wa uwekezaji, tunakazi kubwa kwa vijana kuwatengenezea mazingira ili waweze kufanya vizuri wakati ujao katika maisha yao ya soka.

Kikubwa kwa kila timu ambayo inashiriki mashindano ya kimataifa inapaswa pia kuwatengeneza na vijana wazawa ambao watakuwa na nguvu kesho kupeperusha bendera ya Tanzania.

Ipo wazi kwamba Rashid Juma ambaye kwa sasa yupo zake Polisi Tanzania na Yusuph Mlipili ambaye kwa sasa yupo zake Kagera Sugar walikuwa wanatengenezwa kuwa hazina ya baadaye ndani ya taifa ila mambo kwao yamekuwa magumu.


Ikiwa Simba waliamua kuwaacha basi ina kazi ya kutengeneza wengine ili waweze kupata kitu ambacho kitawafanya kesho wawe na uzoefu kwenye mashindano ya kimataifa.

Kwa Namungo pia ni wakati wao wa kuangalia wale vijana wao ili wakati ujao wawape nafasi. Bado tuna safari ndefu kitaifa na kimataifa.

Kinachotakiwa ni kwa kila timu kuweka nguvu kwenye soka la vijana. Hii itasaidia kuwa na wachezaji wengi wazuri wanaoishi kwenye misingi ya soka.

Pia inapaswa wasiishie kuwa ndani ya timu pekee, wapewe nafasi ya kucheza pia kwenye mechi za ushindani itawasaidia kuweza kwenda na kasi ile ambayo waamuzi wa Bongo wanakwenda nayo.

Tumeona kwamba imekuwa wazi kwenye Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu Bara kote wamekuwa wakikimbilia kwa waamuzi pale mbinu zao zinapokwama kupata matokeo ndani ya uwanja.

Baada ya dakika 90 imekuwa kawaida kwa timu ambayo itashindwa kupata matokeo kuweka egemeo kwa refa. Hii ni ishara mbaya kwa waamuzi wanapaswa waongeze umakini.

Kwenye hili haina maana kwamba waamuzi hawakosei hapana makosa yapo na marefa ni binadamu wana kazi ya kuboresha makosa yao na kufanya vizuri kwa mechi zijazo.

Sheria 17 ni muhimu kufuatwa bila kujali ni mchezo wa aina gani bila kujali ni Simba ama Yanga zipo uwanjani, Kagera Sugar ama Ndanda kote ni muhimu kufuata sheria 17 za mpira.

Malalamiko hayaishi na marefa wanakuwa wakibebeshwa zigo la lawama katika kutimiza majukumu.

Katika hili sio jambo la kukaa kimya na kusubiri ni kitu gani ambacho kitatokea hapo baadaye zaidi ni kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati.

SOMA NA HII  MSIBEBE MATOKEO YENU LEO MFUKONI KWA MKAPA

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) muhimu kusimamia katika hili ili kuona namna gani linaweza kupungua ama kuisha kabisa kwa kuwa kila kitu kinawezekana.

Pia TFF isifumbie macho Ligi Daraja la Kwanza kwa kuwa huku watu wanaishi dunia yao ya kipekee hasa kwenye suala la maamuzi pamoja na usimamizi pia.

Huku ni jikoni kwenye maandalizi ya timu ambazo baadaye zitapanda juu kuleta ushindani mkubwa. Ikiwa kwa sasa hakuna anayejali ambacho kipo jikoni baadaye mambo yatakuwa magumu.

Waamuzi kwa sasa ni wimbo wa taifa kwa kuwa wanaboronga na kuondoa ule ushindani ndani ya uwanja.

Mashabiki pia ambao wanajitokeza uwanjani suala la kubeba matokeo mfukoni hilo pia lisipewe nafasi kwani mpira ni dakika 90.

Pia kwa wadau ambao wanauwezo ni fursa kuwekeza kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza ili kuongeza kipato kwao kwa kuwa timu nyingi zinashindwa kumudu gharama za uendeshaji.

Ikitokea wadau wakazipa sapoti timu itaongeza nguvu kwa wachezaji kupambana ndani ya uwanja kusaka matokeo na hii italeta ushindani kwa timu ambazo zinashiriki ligi kusaka matokeo kwa hali na mali.  

Furaha ya mashabiki ni kuona timu inapata matokeo lakini haiwezi kuwa na furaha ikiwa wataona hakuna kinachoendelea kutoka kwa wachezaji wakiwa ndani ya uwanja iwapo watakuwa hawatoi ile burudani.

Muhimu kila mmoja ambaye atakuwa na nafasi ya kwenda uwanjani kushuhudia burudani basi awe na furaha na kuona kwamba anachokipata ndani ya uwanja ni kile ambacho anakihitaji.

Imani yangu iwapo waamuzi wataamua kusimamia sheria 17 za mpira tutapata timu bora na imara kutoka chini na zikipanda zitaleta ushindani wa kweli.

Kinachowapa furaha mashabiki ni matokeo mazuri hivyo ili matokeo haya yapatikane ni lazima kuwe na maandalizi mazuri kwa wachezaji ili kuwa tayari kwa ajili ya mechi zao zote.

Kila timu kwa sasa inahitaji kupata matokeo mazuri na ili kupata matokeo mazuri ni lazima kila mmoja akachanga karata yake vizuri kwa nafasi yake.

Tunaona pia kuna mechi za Playoff ambazo zinachezwa baada ya ligi kukamilika ila nina ona mfumo unaotumika bado haujawa rafiki.

Timu ambazo zinashiriki kwenye mechi ya kumtafuta mshindi wa Playoff zinakuwa zimetofautiana kwenye madaraja pamoja na muda wa kucheza mechi zao hasa ukizingatia kwamba wengine huwa wanakuwa wamemaliza ligi na kupata muda wa kupumzika.

Hili linapaswa lifanyiwe kazi na TFF kwa kutazama namna mpya ya kumpata mshindi ambaye ataweza kupata ushindi kwa haki bila mazingira ya kutengenezwa kwa kucheza mechi ambazo mshindi anajulikana.

Timu ya Ligi Daraja la Kwanza inapocheza na timu kutoka lligi kuu nafasi kubwa ya kushinda ni kwa yule ambaye yupo ligi kuu hasa kutokana na mazingira yenyewe yalivyo.

Hapa bado umuhimu upo wa kufanya mabadiliko na kuona namna ipi bora itumike kusaka mshindi bila kumkandamiza.