NA SALEH ALLY
NAJUA suala la kuhusiana na klabu kuhakikisha kuwa na vitengo bora na imara vya masoko nimekuwa nikilizungumza mara kwa mara na bado linaendelea kuwa tatizo.
Mazungumzo yangu mara nyingi yanagusa katika namna ambavyo vitengo vya masoko vya klabu vinavyoweza kufanya kazi yake kwa ubora kuhakikisha klabu inaingiza fedha nyingi.
Kuingiza fedha nyingi, kutapimwa na suala la matumizi na mapato. Kwamba klabu fulani inaingiza kiasi fulani cha fedha na inatumia kiasi fulani.
Sahihi ni kuingiza Sh 1,000 na kutumia angalia Sh 600 (huu ni mfano), ndio maana utasikia mwisho wanasema tulipata faida ya Sh 400. Lakini katika klabu za mpira nyingi za hapa nyumbani, zinaingiza Sh 1,000 halafu zinatumia Sh 1,500!
Hili limekuwa likionekana ni jambo la kawaida, kwamba kila mwisho wa mwaka kunakuwa na Sh 500 ambayo inakuwa inazidi katika matumizi na mwisho unaweza kusema kulikuwa na hasara ya Sh 500.
Sasa Sh 500 itapatikanaje, mwisho inakuwa kuna ugumu na klabu inaishia kupata hasara na kubaki katika madeni ambayo yanakwenda yanaongezeka na kuwa sugu. Mwisho ziko klabu kadhaa zimeteremka hadi daraja la kwanza na madeni yake, daraja la pili, la tatu na zipo ambazo zimepotea kabisa katika ramani ya soka.
Unaona ile hali ya watu wengi kuendelea kuamini soka ni burudani au kujifurahisha tu, bado haijaondoka na wanaoiamini baadhi yao ni viongozi katika hizo klabu!
Klabu kuendeshwa kwa hamu au furaha ya wafadhiri, ni kosa kubwa. Ili iwe klabu bora, yenye nguvu na baadaye kubwa, inapaswa kujitegemea kupitia mashabiki wake wanaoiunga mkono.
Mashabiki wanaweza kuwa na faida nyingi kama watatumiwa vizuri na kama watatumiwa kawaida kama ilivyoelekezwa, basi faida yao itakuwa ni pale wanapokwenda uwanjani tu kushangilia, basi.
Kitengo cha masoko kama kinakuwa ni bora, basi hapo ndio unakuwa ndio ule wakati wa kufanya mambo ambayo yanaweza kuwa na faida kubwa kupitia hao mashabiki.
Yako mengi kupitia mashabiki peke yake, kuangalia wanahitaji nini cha klabu na timu yao. Mfano kama ni jezi, fulana, skafu, vishika ufunguo na kadhalika. Inawezekana kabisa angalau kuishawishi au kuingia mkataba na kampuni fulani ikaanza kufanya kazi hizo na klabu kuingiza fedha zake ikiwa inaendelea na mapambano ya ligi.
Uuzaji wa vitu hivyo, utasimamiwa na klabu kwa kushirikiana na kampuni waliyoingia nayo mkataba. Pia kitengo hicho kitaendelea kufanya ubunifu mbalimbali utakaoisaidia klabu kuingiza fedha kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato hata kama itakuwa kidogokidogo.
Makampuni hayawezi kuwa yote yana fedha nyingi lakini bila ubishi makampuni mengi yatakuwa yanataka kujitangaza kupitia mchezo wa soka kwa kuwa yanajua mchezo huo una nguvu na watu wengi.
Yajitangaze vipi, kitengo cha masoko ndiyo kitakuwa na kazi hiyo ya kufanya ushawishi ikiwemo kuyashawishi hayo makampuni kwa kuyaonyesha namna yanavyoweza kufaidika kwa kiasi kikubwa.
Ushawishi wenye ubora, unaweza kuisaidia klabu kupata mikataba na kampuni kadhaa na kuingiza fedha nyingi. Kama itakuwa hivyo, kutakuwa na faida kubwa sana kwa klabu kupata fedha za ziada kupitia wadhamini.
Kuna mengi ya kufanya kupitia kitengo hicho na ushawishi wangu mimi ni kwamba, kuwe na vitengo hivyo na pamoja na kuwa na wazoefu katika masoko, vizuri kiunganishe vijana au watu wanaoujua mpira ili kuweza kuwa na watu wanaoweza kufanya kazi ya masoko kwa kuendana na mpira unavyotaka.