Home Simba SC KOCHA AIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI AFRIKA

KOCHA AIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI AFRIKA


KOCHA mkuu wa klabu ya Simba, Didier Gomes Da Rosa amefunguka kuwa, ana matumaini makubwa ya kukiongoza kikosi hicho kufika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na ubora wa wachezaji alionao.

Gomes alitambulishwa rasmi na Simba kuchukua mikoba ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Sven Vandenbroeck Jumapili ya Januari 24, tayari amekiongoza kikosi hicho katika michezo miwili ya michuano ya Simba Super Cup, akishinda mchezo mmoja na kutoa sare mechi moja.

Leo Alhamisi, Gomes anatarajiwa kuiongoza Simba kwenye mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji.

Akizungumzia uwezo ulioonyeshwa na kikosi chake katika michuano ya Simba Super Cup Gomes amesema: “Kwangu ubingwa tulioupata ni muhimu, lakini jambo la muhimu zaidi ni kuona kikosi changu kikicheza kwa kiwango cha juu katika michezo yetu yote miwili.

“Tuna kikosi chenye hadhi ya kuweza kushindana katika michuano hii mikubwa kwa ngazi ya klabu hapa Afrika, na naamini licha ya mapungufu kidogo ambayo tunapaswa kuyafanyia kazi lakini naamini tutafuzu hatua ya nusu fainali na hata kwenda mbali zaidi ya hapo,”

Simba itaanza kibarua chake kwenye Ligi ya mabingwa Afrika ugenini dhidi ya AS Vita ya DR Congo mchezo utakaopigwa Februari 12 mwaka huu.

SOMA NA HII  BAADA YA KUKIWASHA MECHI YA DAR....NTIBAZONKIZA AWALIA KIAPO AL AHLY MECHI YA MISRI...