Home Yanga SC YANGA KUSHUSHA MUZIKI KAMILI MBELE YA KENGOLD YA MBEYA KESHO

YANGA KUSHUSHA MUZIKI KAMILI MBELE YA KENGOLD YA MBEYA KESHO


 KOCHA Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, amesema haitaidharau timu yoyote atakayokutana nayo kwenye Kombe la FA. 


 

Yanga hivi sasa ipo kwenye maandalizi ya mchezo wa Kombe la FA utakaopigwa kesho, Februari 27 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam dhidi ya Kengold ya Mbeya inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

 

 Kaze amesema hawaifahamu vizuri Kengold, hivyo wataingia uwanjani wakiwa na kikosi kamili na kikubwa ni kuwafunga ili kusonga mbele katika michuano hiyo.


Miongoni mwa wachezaji anaotarajiwa kuwatumia kesho ni pamoja na kinara wa utupiaji ndani ya Yanga, Deus Kaseke mwenye mabao sita, Michael Sarpong,mzee wa spidi 120, Tuisila Kisinda na Feisal Salum.


Kaze amesema kuwa hivi sasa kila mchezo wanauchukulia kama fainali bila ya kuidharau timu yoyote kwani wanataka kutimiza malengo yao msimu huu ambayo ni kubeba ubingwa wa ligi na Kombe la FA.

 

“Kikosi changu kitaingia tofauti katika mchezo wa mzunguko wa nne wa Kombe la FA dhidi ya Kengold ili kuhakikishia tunapata ushindi mnono na kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

 

“Tumepanga kuingia uwanjani katika mchezo huu kama fainali kutokana na umuhimu mkubwa wa pambano hilo kwa lengo la kuvuka katika hatua hii kwenda nyingine.


“Hivyo ni lazima tushinde bila ya kuwadharau wapinzani wetu, nimepanga kutumia wachezaji wangu wote muhimu kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Kaze.


SOMA NA HII  HUYU HAPA MRITHI WA MAYELE, ATAMBULISHWA USIKU MNENE