Home Habari za michezo OSCAR OSCAR:- SIMBA YA BENCHIKHA INAZIDI KUPOTEA…HAIELEWEKI…HAIVUTII NA INARUDI NYUMA..

OSCAR OSCAR:- SIMBA YA BENCHIKHA INAZIDI KUPOTEA…HAIELEWEKI…HAIVUTII NA INARUDI NYUMA..

Habari za Simba leo

SIELEWI! Sio kwa kumkosea heshima. Sio kwa dharau. Sio kwa kukosa adabu. Nilidhani kadri muda unavyozidi kwenda Simba itabadilika kiuchezaji. Niliamini muda unavyozidi kwenda kocha Abdelhak Benchikha ataanza kutengeneza kikosi cha kwanza cha maangamizi, lakini kila nikiitazama Simba sielewi.

Baada ya mechi mbili za kwanza za Benchikha niliona kama kuna mwanga. Simba walicheza vizuri mechi ya ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy. Na kimsingi walistahili kushinda mechi ile, lakini ikamalizika kwa suluhu. Simba walicheza vizuri. Walitengeneza nafasi nyingi za kufunga siku ile.

Baada ya hapo, Simba walikwenda Morocco kucheza na Wydad Casablanca. Pamoja na kuwa walipoteza mechi, lakini waliupiga mwingi. Sasa walionyesha kuimarika. Kila mtu aliyetazama ile mechi alisikitishwa na matakeo kwa sababu Mnyama hakustahili kupoteza.

Kila kitu kwa Mnyama kilionekana kubadilika na kuimarika. Kiasili Simba ni timu inayopenda zaidi mpira wa pasi nyingi. Hii ni falsafa ya klabu. Wanataka kuona mpira mwingi unapigwa. Lakini mara nyingi ili kupata falsafa ya timu ni lazima uanze kwa kupata wachezaji wenye şifa hizo.

Baada ya mapumziko ya mechi za Ligi Kuu na zile za Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ndiyo imenikatisha tamaa. Timu hiyo imeanza kunichanganya. Kila nikiwatazama uwanjani sina hakika kama wanakwenda mbele au wanarudi nyuma.

Kiwango cha Simba kwenye michuano ya Mapinduzi ni aibu tupu. Sikuona cha maana walichokuwa wanakifanya. Hata kama wangeshinda ubingwa, lakini bado isingeleta maana yoyote. Simba ni kama wanarudi nyuma sana kwenye kiwango wanachoonyesha uwanjani.

Baada ya kuwatazama wachezaji waliobaki kwa sababu ya michuano ya Mapinduzi, Simba walitakiwa kuwa kwenye kiwango cha juu. Ni kama wachezaji wanne tu wa kikosi cha kwanza ndio hawakuwepo. Wengine wote walikuwepo, lakini Simba imeendelea kucheza mpira mbovu.

Kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo Simba wanavyozidi kucheza mpira mbovu badala ya kuimarika. Au ni mimi ndiye sitazami vizuri? Nipe maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi wa namna ulivyoona kiwango cha Simba kiuchezaji pale Zanzibar kwenye michuano ya Mapinduzi. Unadhani kinazidi kushuka au kimepanda chini ya Benchikha? Mimi ni kama nimechanganyikiwa. Mwenzenu sielewi elewi. Naona marangi rangi. Ni Kama timu inazidi kupotea. Ni Kama timu haijulikani hata inachezaje kwa falasafa ipi. Nilidhani kadri kocha anavyokaa na timu ndivyo inavyozidi kuimarika. Nilidhani michuano ya Mapinduzi ingemsaidia sana kocha. Lakini kwa kiwango nilichoona sidhani kama imemsaidia chochote. Naona ni kama timu ndiyo inazidi kuchanganyikiwa.

Ukitoa Henock Inonga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Clatous Chama na Kibu Dennis waliojiunga na timu za taifa, wechezaji wengine wote wapo. Wachezaji wote wanaounda kikosi cha kwanza cha Simba siku za karibuni wote wapo. Simba ilipaswa kuonyesha kiwango kizuri. Simba ilipaswa kuwa imeimarika.

Kiukweli kwa kile nilichokiona kwenye michuano ya Mapinduzi ni kama timu imerudi nyuma. Ni kama kumekuwa na hatua nyingi za kurudi nyuma. Hakuna kinachovutia. Hakuna cha kujivunia. Ukimtazama Willy Onana unachoona kwa urahisi kwake labda ni zile tu nywele zake. Hakuwa vizuri sana. Magoli yamepotea. Ukimtazama Jose Luis Miquessone huoni dalili zozote za kurejea kwenye kiwango cha zamani. Timu ni kama imevurugwa. Najua wote tunatazama mpira. Na wewe una maoni yako. Kwa kutumia ujumbe mfupi wa maandishi hebu niambie kipi kimeimarika Simba hii ya Benchikha? Namba yangu ya simu iko hapo juu.

Binafsi sioni chochote. Ni Kama timu inazidi kurudi nyuma. Baada ya mechi mbili za Benchikha niliona dalili njema, lakini kwa sasa naona giza. Sioni dalili ya mwanga.

Pale Simba inaonekana tatizo ni kubwa. Ni tatizo linalohitaji muda mrefu kulitibu. Sio sula la kocha wala mchezaji mmoja mmoja. Karibu kila kitu kinatakiwa kuanza upya. Kila nikitazama timu ya Benchikha kwa sasa najionea giza. Inahitaji muda sana kuipata timu bora.

Kadri siku zinavyozidi kwenda nilidhani timu itaimarika, lakini naona ni kama inazidi kurudi nyuma. Kama sio makosa mengi ya waamuzi, Simba ingetolewa mapema kwenye Mapinduzi. Kifupi, Simba wamecheza mpira mbovu.

Baada ya michuano ya Afcon, Ligi Kuu itarejea. Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika nayo inarejea. Benchikha bado ana kazı kubwa ya kufanya. Simba inahitaji kusonga mbele na njia inaonekana imekaa vibaya.

Ukitazama timu inavyocheza kwa sasa unapata mashaka makubwa. Inasikitisha. Haitii matumaini. Hakuna mahali panapoonyesha Simba imepiga hatua mbele. Safu ya ulinzi bado ni mashaka tupu. Kiungo ukitazama huna uhakika, wala ushambuliaji. Kazi ya ujenzi wa timu ni kama ndiyo imeanza upya.

Pengine kocha anahitaji muda mrefu sana kuleta mabadiliko. Kwa nilichokiona kwenye Mapinduzi kweli ni giza tupu. Sijaona dalili yotote ya timu kuimarika. Kwa ukubwa wa Benchikha wana Simba wanapaswa kuwa watulivu na kutokuwa na matarajio makubwa kwa haraka.

Inaonekana kocha anahitaji muda mwingi. Unamuelewa kweli Kocha Benchikha na namna timu inavyocheza? Nitumie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba ya simu hapo juu.

Makala haya yameandikwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti na Oscar Oscar.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU