Home Habari za michezo BAADA YA KUEPUKA PANGA LA USAJILI….MTIHANI WA CHAMA KWA BENCHIKHA HUU HAPA….

BAADA YA KUEPUKA PANGA LA USAJILI….MTIHANI WA CHAMA KWA BENCHIKHA HUU HAPA….

Habari za Simba leo

HIVI karibuni kulikuwa na taarifa za Simba kutaka kumwacha kiungo wake Clatous Chama, lakini ghafla upepo umegeuka.

Chama ambaye anatajwa kutokuwa kwenye mipango ya kocha wa Simba, Belhack Benchikha, aliingia matata baada ya kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu siku chache kabla Ligi Kuu Bara haijasimama.

Kutokana na tukio hilo la kugomea maelekezo ya kocha msaidizi wa Simba siku ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca, uongozi ulimpeleka staa huyo kwenye kamati ya nidhamu, lakini kumekuwa na usiri mkubwa kuhusu uamuzi uliotokea.

Taarifa zinasema kuwa Simba ilitaka kuachana na kiungo huyo raia wa Zambia, lakini gharama za kuvunja mkataba wake unaomalizika mwishoni mwa msimu zikairudisha nyuma na kufikiri bora kuenda naye hadi mwisho wa mkataba.

Hata hivyo, Chama amebakiza mtihani mmoja tu wa kumshawishi Benchikha na kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ambao ni kupata nafasi na kuwasha moto kwenye kikosi cha Zambia kilichoko katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 huko Ivory Coast na kwa kuanzia leo usiku chama lake la Chipolopolo litavaana na DR Congo kuanzia saa 5:00 usiku.

Endapo Chama atapata nafasi na kuonyesha kiwango cha juu anaweza kumshawishi Benchikha na akamrudisha kwenye kikosi chake kwa kuwa Simba haikufanya usajili kwenye eneo la kiungo huyo huku miongoni mwa waliobaki Msimbazi bado hakuna anayeonekana kuwa bora kama staa huyo.

Hivi karibuni Benchikha alinukuliwa baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi ambao Simba ilichapwa bao 1-0 na Mlandege, akisema timu yake ina tatizo kwenye eneo la utengenezaji mabao (anapocheza Chama ambaye hakuwepo) pamoja na ushambuliaji, lakini uongozi umefanya usajili kwenye eneo moja tu la ushambuliaji.

Sasa mtihani mkubwa umebaki kwa Chama endapo atapata nafasi leo usiku, aonyeshe kiwango cha juu kwenye ubora wake unaofahamika kwa kuwa akifanya hivyo atarudisha imani kwa kocha wake.

Chama amekuwa akitajwa kuwa mmoja kati ya viungo bora zaidi hapa nchini, akiwa anakumbukwa kwa kupiga pasi 16 zilizozaa mabao msimu mmoja wa 2020/2021, akiwa pia anatajwa kati ya viungo wenye mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama Chama akikosa nafasi kwenye michuano hii atakuwa na mtihani mgumu kumshawishi Benchikha kurudi kwenye kikosi cha timu hiyo baada ya fainali za Afcon kumalizika.

SOMA NA HII  HUYU HAPA MRITHI WA KONKANI YANGA