Home news SAKATA LA MWAMUZI KUKATAA GOLI LA GEITA DHIDI YA SIMBA LAPELEKWA KAMATI...

SAKATA LA MWAMUZI KUKATAA GOLI LA GEITA DHIDI YA SIMBA LAPELEKWA KAMATI YA SAA 72…MAREFA WABISHANA…


BAADHI ya waamuzi wa Soka nchini, wametofautiana kuhusu bao la Geita lililokataliwa dakika ya 87 dhidi ya Simba juzi usiku kwenye Uwanja wa Mkapa wakidai kwamba ilipaswa kumalizika bao 2-2. 

Martin Saanya alikataa bao la mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole kwa kile alichodai kuwa alimfanyia madhambi beki wa Simba, Shomari Kapombe kabla ya kupiga kichwa mpira huo na kufunga.

 Waamuzi wawili maarufu nchini ambao wameomba majina yao yahifadhiwe kwa kuhofia kuadhibiwa wamekiri kwamba lilikuwa ni bao na mechi ilitakiwa kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 na si mabao 2-1.

“Vitu vingine havitakiwi kuzungumzwa sana, ila sijui mwamuzi alilikataa goli lile kwa sababu gani, lakini binafsi naliona lilikuwa ni bado halali kwa Geita,” alisema mmoja wa waamuzi kutoka Tanga ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake.

Mwamuzi mwingine wa Tabora alisema hakukuwa na kuotea wala faulo. “Nililijadili goli lile na mwamuzi mwenzangu lilikuwa ni halali kwa asilimia 100, hakukuwa na mgongano kati ya mchezaji wa Simba na Geita, wala kugusana kwa aina yoyote, huwezi kusema lile halikuwa bao halali,”alisema.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti ilizipata Jijini Dar es Salaam jana ni kwamba sakata hilo litajadiliwa muda wowote kwenye kamati ya saa 72.

Othman Kazi mwamuzi wa zamani wa Tanzania, ameungana na Saanya kusisitiza halikuwa bao halali.

“Alipopuliza filimbi Aishi (Manula) na Onyango (Joash) walisimama, lakini kwa kuwa mchezaji alikuwa kwenye mwendo ndiyo sababu alifunga,” alisema Othman ingawa ametofautiana na wengine wawili ambao wamedai lile lilikuwa ni bao halali kwa Geita.

Jana bosi wa Simba, Murtaza Mangungu alisema; “Ile haikuwa mieleka ni soka, kama ingekuwa ni mieleka basi ingekuwa goli kwa Geita.”

Kocha msaidizi wa Geita, Fred Felix Minziro alibainisha kusikitishwa; “Kila mtu ameshuhudia kilichotokea, ambaye hakupata nafasi ya kulishuhudia tukio hilo akajipe muda kuliangalia, hata hivyo nawapongeza wachezaji wangu kwa kupambana.”

Makamu mwenyekiti wa kamati ya waamuzi, Israel Nkongo alisema; “Kuhusu kamati ya saa 72 hiyo sifahamu, ni kama tayari tunatoa uamuzi, lakini ukiangalia video inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii, haionyeshi tukio lote hadi mwamuzi kulikataa bao lile. Binafsi sikuwa uwanjani, lakini ukiangalia video inayosambaa, si video sahihi ya kutolewa uamuzi, tutakaa kuangalai video yote kuanzia tukio linaanza hadi refarii kulikataa hilo goli,” alisema mwamuzi huyo.

SOMA NA HII  POLISI TZ WAIKALIA YANGA KOONI KUELEKEA MECHI YA KWANZA YA LIGI KUU...WAKUMBUSHIA KIPIGO CHA VIPERS...