HUKU kikosi cha Simba kikiwa kimerudi nchini leo mchana kikitokea Morocco kilipokuwa kimeweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa, Siku ya Tamasha la Simba (Simba Day) Septemba 19, mwaka huu, kitashusha Mabingwa Afrika kucheza nao mechi ya kirafiki, imefahamika.
Akizungumza jijini jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema baada ya kurejea nchini, wachezaji watapewa mapumziko ya siku mbili na Jumanne wataingia kambini kwa ajili ya maandalizi mengine ya msimu mpya ‘Pre Season’.
Alisema kikosi kitaondoka Dar es Salaam na kwenda moja ya mkoa uliokuwa tulivu na mazingira mazuri kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya msimu mpya kwa kucheza mechi za kirafiki na timu za Ligi Daraja la Kwanza na zile zinazoshiriki Ligi Kuu.
“Ni wapi tutaenda kuweka kambi, hilo litawekwa wazi baadaye, ila Jumanne wachezaji ambao hawako katika majukumu ya timu ya taifa, wataingia kambini na kujiandaa kwa ajili msimu mpya,” alisema Kamwaga.
Hata hivyo, Kamwaga alipoulizwa kuhusu mechi ya kirafiki ya kimataifa watakayocheza Simba Day Septemba 19, mwaka huu, alisema ipo kamati inayoshughulikia na bado hajafikishiwa mezani kwake na akiipata ataiweka hadharani.
Lakini chanzo chetu ndani ya kamati hiyo, kilitueleza kwamba wanatarajia kucheza na timu moja kubwa iliyowahi kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tutacheza na timu moja kubwa iliyowahi kutwaa Ligi ya Mabingwa Afrika, siwezi kuitaja kwa sababu ndiyo kwanza tupo kwenye mazungumzo, lakini pia Simba ina utaratibu wake wa kutoa taarifa si kila mmoja anaruhusiwa kuzungumza, mtafute Kamwaga atakueleza kama limeshamfikia,” kilisema.
Tayari Simba imecheza mechi mbili za kirafiki ikiwa kambini nchini Morocco dhidi ya FAR Rabat iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-1 na kisha kutoka kufungana bao 1-1 dhidi ya Olympique Club de Khouribga.