TIMU ya Yanga imetangaza kuanza rasmi ukarabati wa jengo lao lililopo Mtaa wa Jangwani,Dar es Salaam ambapo ndio makao makuu ya klabu hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo kwenye makao makuu hayo, mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msola amesema ukarabati huo utaanza rasmi kuanzia leo Machi Mosi na yote hayo yatakamilishwa na watu watakaojitolea.
“Tunaenda kufanya ukarabati wa jengo letu kuanzia leo na tunatarajia kuanza na vyumba vya kuishi wachezaji wa timu zetu za vijana na wanawake ili kupunguza gharama za kambi.
Ukarabati huo utafanywa na wadau waliojitoa ikiwemo baadhi ya matawi na watu binafsi pia tunakaribisha watu wote watakao wiwa kuchangia ukarabati huu ambao tunataka ukamilike mapema iwezekanavyo,” amesema Msola.
Pia mwenyekiti wa kamati ya miundombinu ya Yanga mhandisi Bahati Mwaseba ametolea ufafanuzi ukarabati huo na kuonyesha chumba kimoja anbacho wamekikarabati kama mfano.
“Huu ni mkakati wa kuhakikisha jengo letu linakuwa safi na la kisasa, tunaanza na vyumba ambavyo watakuwa wakiishi wachezaji wetu ambavyo ni 30 na baada ya hapo maeneo mengine yatafuata.
“Tayari tumekarabati chumba kimoja cha mfano na gharama yake ni shilingi milioni sita (6,000,000) hivyo kila chumba kinahitaji gharama hiyo ili kukamilika,” amesema Mwaseba.
Sambamba na hao pia alikuwepo mwenyekiti wa tawi la Yanga Eliti lililopo mikocheni ambaye alizungumza kwa niaba ya matawi ya timu hiyo.
“Tutachukua baadhi ya vyumba na tutavifanyia ukarabati, hii ni timu ya Wananchi na Wananchi wenyewe ni sisi hivyo lazima tuifanye iwe na muonekano safi,” amesema Zabroni na kuongeza:
“Kila mwenye uwezo aje tuungane kukarabati jengo letu na tuoneshe uYanga wetu, haipendezi kwa timu kubwa kama hii kuwa na jengo lisiloridhisha,” amesema.
Ukarabati huo utajumuisha vitanda vya kisasa, runinga na friji ndogo ndani ya chumba na kila atakaye au watakao jitolea kufanya ukarabati huo litaandikwa majina yao mlangoni kwa juu kama kumbukumbu.