Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefungua tenda ya kuandaa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo yanaanza kwa mara ya kwanza mwaka huu
Mashindano hayo yatashirikisha jumla ya timu saba zitakazofuzu kutoka katika kila kanda ya soka iliyo chini ya CAF pamoja na timu ya nchi itakayoandaa mashindano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CAF leo, mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake yatafanyika kati ya mwezi Oktoba, Novemba au Disemba kulingana na uamuzi wa mwisho utakaotolewa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo.
“CAF imefungua tenda kwa nchi kwa uandaaji wa mashindano ya ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2021.
Vyama vya nchi vinaombwa kuwasilisha maombi ya tenda zao yakiambatana na viwanja (viwili vinahitajika) na vile vya mazoezi (angalau viwanja vinne vya mazoezi), malazi (yanayotosheleza kwa timu nane) na uhakika kutoka serikalini.
Tarehe ya kufungwa kwa maombi ni Machi 31, 2021,” ilisema taarifa hiyo ya CAF.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake kuchezwa yakiwa na lengo la kukuza soka la wanawake barani Afrika.
Kuanzishwa kwa mashindano hayo kunaweza kuwa fursa nzuri kwa Tanzania ambayo kwa muda wa miaka mitano sasa imekuwa na Ligi Kuu ya Wanawake.
Kwa sasa, ligi hiyo ya Wanawake Tanzania inaongozwa na timu ya Yanga Princess yenye pointi 38, ikifuatiwa na Simba Queens yenye pointi 35 wakati JKT Queens iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33.