KASHINDWA kujizuia. Ndio, dada wa bilionea na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Mo Dewji, Fatema anayeisimamiwa kwa sasa Simba Queens, ameeleza kukoshwa na straika wa Wekundu wa Msimbazi, Meddie Kagere.
Kagere, aliye moto tangu ajiunge na timu hiyo misimu mitatu kutoka Gor Mahia ya Kenya mwaka 2018 na kuifungua mabao 69 ya kimashindano yakiwamo 53 ya Ligi Kuu Bara, umahiri wake uwanjani umemfanya Fatema kukiri amekuwa akimkuna vilivyo ndani ya kikosi hicho.
Fatema aliliambia gazeti la Mwanaspoti katika mahojiano maalumu kwamba Kagere ni mchezaji anayejipambanua tofauti na nyota wengine wa timu hiyo inayoiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika. “Kiukweli miongoni mwa wachezaji ninaowakubali Simba ni pamoja na Meddie, unaweza kuniuliza kwanini? Ni kwa sababu yupo tofauti kimtazamo na wachezaji wengine wengi,” alisema.
“Ujue nimewahi kupata nafasi ya kuongea mawili matatu na Meddie. Anajitambua sana, nilichokiona kingine kwake ni kwamba amekuwa mstari wa mbele pia katika kutekeleza majukumu yakiendana na muda.”
Straika huyo anaongoza kwa mabao katika Ligi Kuu Bara sambamba nahodha wake, John Bocco.