Home Yanga SC KAZE :- YANGA SC BILA YA NTIBAZONKIZA NA YACOUBA WASAHAU UBINGWA VPL

KAZE :- YANGA SC BILA YA NTIBAZONKIZA NA YACOUBA WASAHAU UBINGWA VPL


Kocha aliyetemwa na Yanga, Cedric Kaze amesema bila wachezaji wawili wa kigeni, Saido Ntibazonkiza na Yacouba Sogne kurudi kwenye ubora wao, timu hiyo itakuwa na wakati mgumu.

Kaze raia wa Burundi alitemwa na Yanga wiki iliyopita pamoja na benchi lake lote la ufundi kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo inayoongoza ligi kwa pointi 50.

Akizungumza jana kwa mara ya kwanza hadharani  tangu atimuliwe, Kaze alisema Yanga ni nzuri, lakini ujio wa Burundi na Yacouba, ambao walikuwa majeruhi ni muhimu kikosini.

“Huwa sipendi sana kuzungumzia mchezaji mmoja mmoja, lakini kwa hali iliyopo kwenye kikosi kwa sasa nguvu ya Saido na Yacouba inahitajika sana, ni wachezaji ambao wana uzoefu mkubwa na wakiwepo wanaongeza morali kikosini,” alisema Kaze, ambaye huenda akaondoka Dar es Salaam kesho kwenda kwao Burundi kusalimia kabla hajakwenda Canada yalipo makazi yake.

“Wakikosekana hao safari ya ubingwa wa Yanga itakuwa ngumu kidogo, hata wakiwa kwenye timu unaona kabisa na kiwango cha kujiamini kwa baadhi ya wachezaji kinapanda zaidi na unaona timu inacheza kwa nguvu zaidi, vitu kama hivyo ni muhimu zaidi kwenye timu kuelekea kwenye safari ya ubingwa muda kama huu.

“Wote hao wawili majeraha yao yanaendelea vizuri, wakirejea kutakuwa na tofauti kubwa na ndicho kitu ambacho tulikuwa tunakitarajia kabla haya mambo hayajatokea,” alisema Kaze, ambaye alikiri kwamba kuna baadhi ya mambo alikuwa anaingiliwa kiutendaji na baadhi ya viongozi licha ya kwamba hakuwataja.

“Yanga hii kama makocha watakaokuja wakiendelea na ile mipango tuliyokuwa nayo sisi wana uwezo wa kubeba ubingwa, muhimu ni kuangalia usipitwe na Simba mpaka siku ambayo unakutana nayo na ukiikuta uifunge au kutoa sare kama tulivyofanya sisi.

“Ukikubali Simba ikikupita kirahisi itakuwa tatizo kidogo na ngumu kutetea ubingwa,” alisema Kaze na kukiri kwamba Simba ina faida ya kikosi kipana kuliko Yanga, lakini morali ya wachezaji wake na mipango waliyokuwa nayo iliwapa ugumu Msimbazi.

Kaze, ambaye amekiri kupata ofa tatu Afrika, amekutana na Simba mara mbili ambapo moja ilikuwa sare kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na Mapinduzi akawapiga Simba na kubeba kombe.

SOMA NA HII  MWAMNYETO AFUNGUKA KILICHOFANYIKA VYUMBANI WAKATI WA MECHI YA SIMBA JUZI..."MAMBO YANGEKUWA MAGUMU"...

Balaa kwa kibarua cha Kaze kilianza katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, baada ya kuvuna pointi saba katika michezo sita iliyoshuka uwanjani.

Baada ya kutoka katika kipigo cha kwanza cha Yanga msimu huu, Kaze aliiongoza miamba hiyo ya Jangwani kuivaa Polisi Tanzania, ambao bao lao la dakika za mwisho la kusawazisha lile la Fiston Abdulrazack lilihitimisha miezi yake mitano kuinoa timu hiyo.