Home Simba SC MO DEWJI AWEKA MILIONI 230 MEZANI KUWAUA EL MERREIKH LEO

MO DEWJI AWEKA MILIONI 230 MEZANI KUWAUA EL MERREIKH LEO


BILIONEA kijana nchini, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ameweka mkwanja mrefu katika mechi ya leo Jumanne ambayo Simba itakuwa nyumbani kuikaribisha El Merreikh ya Sudan katika Uwanja wa Mkapa.

Hiyo ni mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo awali timu hizo zilitoka sare tasa.

Katika kuhakikisha wanavuna pointi tatu dhidi ya wapinzani wao, Mo Dewji ameweka Dola za Marekani 100,000 ambazo ni zaidi ya Sh230 milioni. Pesa hizo ni kwa ajili ya kuongeza morali na motisha kwa wachezaji kupambana ili kupata ushindi ambao utawapa alama tatu na kufikisha pointi 10 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa vinara wa kundi A.

Baada ya mchezo huo watabakiwa na michezo miwili dhidi ya AS Vita ambao watacheza nao Dar na ule wa mwisho na Al Ahly watakaowafuata Misri.

Mkwanja huo ambao unatolewa kama motisha utagawanywa katika makundi matatu – wachezaji watakaocheza watapata si chini ya Sh10 milioni, watakaokuwa benchi si chini ya Sh5 milioni na watakaokuwa jukwaani kifuta jasho.

Simba kama ikishinda me-chi hiyo itakuwa na uhakika wa kucheza robo fainali huku ikisubiri matokeo ya mechi kati ya AS Vita ambayo itakuwa nyumbani (DR Congo) dhidi ya Al Ahly- zote zikiwa na pointi nne.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema wachezaji wake wote waliokuwa kambini wana morali ya kucheza mechi hiyo ili kuhakikisha wanavuna pointi tatu muhimu kwao.

“Ambavyo tulicheza katika mechi ya kwanza na Merrikh kule kwao kwa kujilinda zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza itakuwa tofauti na ambavyo tutacheza mchezo huu wa nyumbani,” alisema Gomes.

UONGOZI WAJIPANGA

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mulamu Ng’hambi alisema kila kitu kimekamilika kwa ajili ya mechi hiyo.

“Kuhusu bonasi ni jambo la kawaida kwa timu yetu kuanzia mechi za ligi na hata michuano hii ya kimataifa, wakishinda, wakitoka sare kuna viwango tofauti vya pesa ambavyo wanavipata,” alisema Mulamu.

“Simba iko tayari kwa mchezo, hatuna wasiwasi wala shida ya aina yoyote ile, kila mchezaji tunaamini atapambana kuhakikisha timu inapata matokeo katika mchezo huo wa nyumbani.”

SOMA NA HII  AHMED ALLY AWACHONGEA YANGA TFF...USHINDI WAO UCHUNGUZWE...ATEMA CHECHE HIZI

Kuhusu Simba kucheza bila mashabiki, Mulamu alisema kuwa: “Hata michezo iliyopita ugenini dhidi ya AS Vita na Al Merrikh tulicheza bila mashabiki na kupata matokeo mazuri, hivyo hata sasa tutapambana hivyohivyo.

“Tunachoumia ni mashabiki wetu kukosa nafasi ya kuiona timu yao ikiwa uwanjani, lakini kwa timu haijaathirika kwa lolote lile zaidi ya mashabiki ndio wameumizwa sana na katazo hilo la CAF.”