Home Ligi Kuu LUNYAMILA: WAAMUZI MSITURUDISHE TULIKOTOKA

LUNYAMILA: WAAMUZI MSITURUDISHE TULIKOTOKA


LIGI Kuu Bara pamoja na michuano mbalimbali iliyo chini ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF), imesimama kwa muda kupisha michezo ya kimataifa iliyo kwenye kalenda ya Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA).

Ipo michezo michache ya ligi hiyo ambayo kwa sababu maalum imeendelea kuchezwa. Kwa mahali ambapo ligi imefikia unaweza kusema utamu umezidi kuongezeka, hii ni kwa sababu huu ndiyo mzunguko wa kuweka sawa hesabu na kuvuna matunda ambayo timu ziliyapanda tangu kuanza kwa msimu.

Ukiangalia msimamo wa ligi, utagundua kuwa vita ni kubwa sana katika maeneo mawili ambayo ni kwa wale wanaochuana kusaka taji la ubingwa, ambapo Simba na Yanga zinapewa nafasi kubwa licha ya kwamba Azam nao kwa sasa hawapo mbali.

Lakini vita nyingine kubwa ni ile iliyopo chini mwa msimamo ambapo zipo timu zinapambana kuhakikisha hazishuki daraja, bali zinasalia kuwa sehemu ya ligi kwa msimu ujao wa 2020/21.

Kama ilivyokuwa mwaka jana, mwaka huu timu nne zitashuka moja kwa moja huku mbili zikicheza hatua ya mtoano.

Hapa ndipo kasheshe linapoanzia, kwani kila mmoja anapambana kutokuwa sehemu ya watakaopotea, bali anarudisha matumaini na kutetea eneo analotoka. Katika hali kama hii, ishu ya umakini kwa wasimamizi wa ligi inapaswa kupewa kipaumbele sana.

Hii ni kwa sababu zipo klabu ambazo zinaweza kuonewa kwa kuwa tu zinakosa misuli katika hali zao za uwekezaji na uchumi.

Kwa bahati mbaya mara nyingi yanapotokea mambo kama hayo taaluma ya Waamuzi hugusiwa zaidi, ambapo wamekuwa wakituhumiwa kushindwa kusimamia kwa uhakika sheria 17 sa soka.

Hali hii kwa hapa nchini imedhibitiwa kwa kiwango fulani kulinganisha na siku za nyuma, lakini bado kuna maeneo yanaonekana kulega, kuna wakati msimu uliopita Waamuzi walishutumiwa sana kutokana na makosa ya kujirudia katika kila mchezo.

Hali hii kuna wakati ilioanishwa na changamoto ya mazingira ya kufanyia kazi, ikiwemo kukosekana kwa malipo ya stahiki zao kwa wakati, na wakati mwingine mapungufu yao ya kibinadamu.

SOMA NA HII  SAMATTA:TUTAKUJA KIVINGINE MBELE YA SIMBA

Ni kweli Waamuzi hawa sio Malaika hivyo, ni wazi wanaweza kufanya makosa, lakini hata kama wanafanya makosa basi haipaswi kuwa ya kujirudia.

Bado kuna changamoto ya ubora kwa waamuzi wetu, na hili limekuwa likithibitishwa mara kwa mara na malalamiko mengi ya wadau wa soka hapa nchini, na hata kupitia adhabu zitolewazo na bodi inayosimamia uendeshwaji wa ligi kuu (TPLB).

Tujiulize tunawezaje kulipunguza kama sio kuliondoa kabisa tatizo hilo, kwa kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo mafunzo, kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza vifungu vya adhabu kwa waamuzi watakaokiuka miiko ya kazi.

Hii inaweza kutusaidia kuondokana na changamoto za maamuzi na kutusaidia kuwa ligi iliyo bora. Hivyo chonde Waamuzi msiturudishe tulikotoka.