UONGOZI wa Yanga, umeweka pembeni mchakato wa kumpata kocha mkuu mpya wa timu hiyo, atakayekuja kuchukua nafasi ya Mrundi, Cedric Kaze, huku kibali kikitajwa ndiyo sababu kubwa.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu watangaze kuachana na Mfaransa, Hubert Velud waliyekuwa naye katika hatua za mwisho za kukamilisha mipango ya kumnasa.
Yanga iliachana na Velud baada ya kushindwana katika maslahi ikiwemo mshahara na fedha ya uhamisho kabla ya Yanga kutua kwa makocha wengine watatu ambao mmoja wapo atamrithi Kaze.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Kamati ya Ufundi ya Yanga iliyo chini ya Dominic Albinius, itakutana Jumamosi hii tayari kwa ajili ya kumuandalia tiketi kocha huyo atakayepitishwa.
Mpaka sasa, kocha anayetajwa zaidi ni Sebastian Migne aliyewahi kuzifundisha timu za taifa za Kenya, DR Congo na Guinea Ikweta. Mwingine ni Mserbia, Nikola Kavazovic.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, wamepanga kumchukua kocha mwenye uwezo na uzoefu wa soka la Afrika, hivyo katika kikao hicho kamati hiyo ndiyo itaamua kocha yupi watakayempa timu.
“Ofisi zote za wizara mbalimbali hivi sasa zimefungwa kutokana na kubanwa na majukumu ya msiba wa Rais Magufuli, hivyo ni ngumu kwa kocha huyo mpya kupata kibali wakati nchi ikiwa katika maombolezo.
“Tumepanga kocha atakayekuja aanze kazi moja kwa moja, hivyo tumeona tusubirie mazishi ya Rais Magufuli yapite ili tumalizie mchakato huo uliokuwa katika hatua za mwisho.
“Kilichobaki ni kumtangaza pekee kwani tayari tunayo majina matatu ya makocha ambao CV tumezipitia na kushawishiwa nazo, hivyo mmoja wapo ndiye atakuwa kocha, hivyo hadi kufikia Jumamosi atakuwa tayari ameshajulikana kwani siku hiyo kamati hiyo ya ufundi itakutana,” kilisema chanzo.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla kuzungumzia hilo, alisema: “Hivi sasa nchi ipo kwenye maombolezo ya msiba mkubwa wa Rais Magufuli, hivyo kila kitu kimesimama hadi tutakapomzika shujaa wetu Magufuli, hivyo Wanayanga wawe watulivu katika kipindi hiki,” .