UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa bado heshima ya Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli itazidi kuishi kutokana na mambo makubwa ambayo ameyafanya kwa taifa la Tanzania.
Maguli aliyetangulia mbele za haki Machi 17,2021, Machi 26 alipumzishwa kwenye makazi yake ya milele, Chato mkoani Geita katika makaburi ya familia ya Magufuli.
Kuondoka kwake kumeacha simanzi kwenye mioyo ya Watanzania pamoja na Waafrika kwa sababu alikuwa ni mtetezi wa wanyonge, mpenda haki bila kusahau kutekeleza majukumu yake kwa wakati.
Furaha yake kwenye michezo ilikuwa ni kuona timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inashinda huku kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara maono yake ilikuwa ni kuona kwamba siku moja timu moja inatwaa Kombe la Afrika, (Ligi ya Mabingwa Afrika).
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit, amesema kuwa Magufuli alikuwa ni kiongozi shujaa na mwenye msimamo katika kusimamia kile anachokiamini.
“Magufuli alikuwa ni kiongozi makini na mwenye msimamo, atakumbukwa kwa kuwa mengi aliyokuwa akiyafanya yanaonekana na yanaleta matokeo kwa kila Mtanzania.
“Ukianza na kuruhusu kuanza kwa michezo mapema kwa timu zote za bara la Afrika haikuwa jambo jepesi ila aliamini inawezekana wakati ule wa janga la Corona.
“Tanzania ilikuwa ni nchi ya kwanza kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani na mechi zikaendelea kama kawaida ambapo kuna mataifa mengine yalifuta ligi zao na nyingine zilisismamisha ligi kwa muda mrefu na ziliporudi mashabiki hawakuruhusiwa kuingia,” amesema.