ZIKIWA zimesalia siku chache kufikia siku ya mtanange kati ya Simba na AS Vita, Kocha Mkuu wa AS Vita kutoka nchini DR Congo, Florent Ibenge ameweka wazi kuwa ratiba yake ya sasa si rafiki kwa klabu hiyo kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba.
Ibenge ukiachana na kuwa kocha wa AS Vita, pia ni kocha mkuu wa kikosi cha timu ya taifa ya Congo ambapo Jumatatu aliongoza taifa la Congo katika mchezo wao wa mwisho wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika dhidi ya Gambia.
Kwenye mchezo huo Ibenge alishuhudia kikosi chake kikishinda bao 1-0 ila kilikwama kufuzu Afcon nchini Cameroon kwa kuwa kipo nafasi ya tatu.
Ibenge amesema kuwa ratiba ya mechi za timu za taifa na michuano ya Ligi ya Mabingwa imebana sana kiasi cha kukosa siku za kutosha kwake kukiandaa kikosi cha AS Vita kuelekea mchezo wao unaofuata wa michuano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Simba.
“Ratiba si rafiki kwetu, nadhani hii ni kwa klabu nyingi zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa, ukiangalia mechi za timu za taifa na ile michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa klabu imebana, hakuna muda wa kuweza kuiandaa timu vizuri.
“Wachezaji wengi wa klabu wanakuwa kwenye majukumu ya timu ya mataifa yao, hivyo hawatakuwa na muda wa kujiandaa vizuri, kwangu pia hivyohivyo, kwa sasa nipo timu ya taifa lakini kwa wakati huo natakiwa niiandae AS Vita katika mchezo dhidi ya Simba, kwa kweli ratiba haipo salama kwangu na kwa wachezaji wetu,” amesema Ibenge.
Simba na AS Vita zinatarajiwa kumenyana Jumamosi hii Aprili 3 katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar kwenye mchezo wa marudiano ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mchezo wa awali uliofanyika Congo DR, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, likifungwa na Chris Mugalu kwa penalti mara baada ya beki wa AS Vita Ousmane Outarra kushika mpira uliopigwa na Luis Miquissone.