Home Simba SC SIMBA: AS VITA HAWATOKI

SIMBA: AS VITA HAWATOKI

KIKOSI cha klabu ya Simba kinaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wao wa Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita kutokea DR Congo, huku wakitamba kuwa wanazitaka pointi tatu za mchezo huo.

Aprili 3, mwaka huu Simba inatarajia kuwavaa AS Vita katika mchezo wao wa tano wa hatua ya makundi utakaopigwa kwenye uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam.

Simba inaongoza msimamo wa kundi A, ambapo mpaka sasa wamekusanya pointi 10 baada ya kucheza michezo minne, wakishinda michezo mitatu na kutoa sare mchezo mmoja.

Simba inahitaji pointi moja tu katika michezo miwili iliyobaki ili kuweza kufuzu hatua ya robo fainali, lakini matokeo ya ushindi yatawafanya wawe katika nafasi nzuri ya kumaliza vinara wa kundi hilo.

Akizungumzia mipango yao, Meneja wa kikosi cha klabu ya Simba, Patrick Rweyemamu alisema: “Kikosi cha wachezaji wetu ambao hawajajumuishwa katika vikosi vya timu za taifa, kinaendelea na mazoezi kila siku chini ya kocha mkuu Didier Gomes.

“Tunajua ugumu na umuhimu wa kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huu, mpaka sasa hakuna mchezaji yeyote aliye na majeraha hivyo tunachosubiri ni kurejea kwa sehemu ya wachezaji wetu walio kwenye vikosi vya timu ili kocha afanye maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo huo ambao ni wazi tunahitaji ushindi,”

SOMA NA HII  BOCCO KUONGOZA MASHAMBULIZI DHIDI YA WABOTSWANA LEO..KIKOSI KAMILI HIKI HAPA